Baraza la Madiwani Manispaa ya Ubungo limepitisha makisio ya mpango wa bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 yenye jumla ya Tsh 109,449,392,100 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ruzuku ya mishahara na matumizi mengineyo.
Baraza limepitisha mapitio hayo kwenye mkutano maalumu wa baraza la Madiwani uliofanyika leo februari 10, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo na kuweka msisitizo wa kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kufikia malengo.
Akiwasilisha rasimu ya makisio ya mpango na bajeti ya Halmashauri hiyo Ndg. Andambike Kyomo Mchumi wa Manispaa hiyo alifafanua kuwa jumla ya bajeti hiyo ya shilingi 109,449,392,100 imejumuisha shilingi 74,838,346,000 ambayo ni ruzuku kutoka Serikali kuu, shilingi 34,520,402,100 ni fedha za makusanyo ya ndani ya Halmashauri na shilingi 90,644,000 ni fedha kutoka kwa wafadhili.
Kyomo ameendelea kufafanua kuwa kiasi cha shilingi 74,838,346,000 ambacho ni fedha za ruzuku kutoka Serikali kuu zinajumuisha kiasi cha shilingi 62,341,057 ikiwa ni mishahara, shilingi 1,278,545,000 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi 11,218,744,000 kwa ajili ya miradi ya maendeleo toka Serikali kuu.
Kiasi cha Shilingi 34,520,402,100 ambacho ni fedha ya mapato ya ndani inajumuisha kiasi cha shilingi 22,059,738,000 ni mapato halisi, kiasi cha shilingi 11,635,664,100 ni mapato lindwa na kiasi cha shilingi 825,000,000 ni michango ya wananchi.
Sambamba na hayo Kyomo amesema bajeti hiyo imazingatia vipaumbele sita ikiwemo kuboresha makusanyo ya mapato ya ndani, kuboresha miundombinu ya elimu, uboreshaji wa huduma na miundombinu sekta ya afya, kuimarisha utawala bora, kuboresha miundombinu ya barabara na kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na utoaji taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Akihitimisha Mhe. Nyaigesha amemshukuru Mhe Rais kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo na uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya 10% na kuahidi kuwa bajeti ya 2023/2024 Manispaa itaenda kutekeleza miradi itakayoenda kutatua kero za wananchi katika nyanja mbalimbali
Aidha, Mstahiki Meya amesema ukusanyaji wa mapato utafanyika kwa ufanisi kwa kila mtu kushiriki ipasavyo na kusimamia sheria ndogo mpya za Manispaa hiyo
“Kwa mara ya kwanza Halmashauri yetu inaanza kutumia sheria ndogo zake mpya ambazo zimetungwa na baraza la Manispaa ya Ubungo badala ya zile za Kinondoni ambazo tulikuwa tukizitumia muda wote” alisema Mstahiki Meya.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa