Ni maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa darasa la Kwanza na kidato cha kwanza mwaka 2022.
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo inatarajia kutumia shilingi bilioni 2 fedha za mapato ya ndani kujenga na kukarabati vyumba vya madarasa 100 kwa shule za Msingi na Sekondari za Manispaa hiyo ikiwa ni maandalizi ya kuwapokea wananfunzi wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza mwaka ujao wa 2022.
Ujenzi huo wa vyumba 100 vya madarasa unaotarajia kuanza Agosti mwaka huu na kukamilika Novemba 20, 2021, unalenga kuboresha miundombinu ya shule na hivyo kuwana mazingira bora ya kujifunza na kujifunzia.
Akizungumza na Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kwenye kikao kazi kuhusu utekelezaji wa mpango huo kwa kwaka wa fedha 2021/2022, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Beatrice Dominic amewataka wasimamizi wa miradi hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano na umakini mkubwa huku wakifuata kanuni, taratibu na miongozo ya serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Beatrice amewaeleza wasimamizi wa miradi hiyo kuwa, Miradi hiyo inajengwa kwa kufuata mwongozo wa “Force account” hivyo wahakikishe wanauzingatia vizuri hususani kununua vifaa viwandani pamoja na kuwa na watoa huduma tofauti tofauti wa vifaa ili kupunguza gharama ya mradi lakini kupata vifaa kwa wakati.
“hili zoezi ni la kimkakati hivyo tujipange kulitekeleza kwa wakati, uadilifu na kuzingatia taratibu na mwongozo ili ifikapo Novemba 2021 miradi yote iwe imekamilika”alisisitiza Beatrice
Akiwasilisha Mpango wa ujenzi wa miundombinu hiyo, Mkuu wa Idara ya Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji ndugu, Salvius F. Nkwera ameeleza kuwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Manispaa imetenga jumla ya shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule na huduma za afya ambapo bilioni 2 ni kwa ajili ya madarasa na bilioni 1.5 ni kwa ajili ya ujenzi wa vituo 3 vya afya.
Aliendelea kueleza kuwa, Ujenzi wa miundombinu ya shule ni kati ya vipaumbele kumi vitakavyotekelezwa kwenye bajeti ya mwaka fedha 2021/22 kwa kutumia fedha za mapato ya ndani kama sehemu ya kuboresha utoaji huduma kwa wananchi wake.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa