Kufuatia uundaji wa Bodi na Kamati mpya za ushauri kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, Manispaa ya Ubungo imewapa semina elekezi wajumbe wa Bodi na Kamati hizo lengo ikiwa ni kuwajengea uelewa wa wajibu na majukumu yao kama chombo kinachounganisha jamii na Serikali katika uboreshaji wa utoaji wa huduma za afya kwa Wananchi.
Akiongea wakati wa kufungua semina hiyo, Mganga Mkuu wa Manispaa Dkt Peter Nsanya ameeleza kuwa baada ya kuundwa kwa bodi na kamati mpya Manispaa imeona itoe semina elekezi kwa wajumbe juu ya wajibu na majukumu yao ikiwemo kusimamia utoaji wa huduma bora za afya kwenye vituo wanavyoviwakilisha.
"Kama kuna malalamiko kwa wananchi juu ya utoaji wa huduma ni wajibu wenu kuyachukua na kuwasilisha kwenye vituo na baada ya kufanyiwa kazi rudisheni mrejesho kwa wananchi ili waone kero zao zinatatuliwa" alieleza Nsanya.
Aidha, wajumbe wamekumbushwa kuwa ili wawe wajumbe hai kwenye kamati zao ni lazima wawe wamejiunga na moja ya bima za afya ikiwemo iCHF ili waweze kuhamasisha jamii kujiunga na bima kwa vitendo.
“Kwa wale wasio na bima wajiunge haraka" alisisitiza Nsanya
Aidha wajumbe wamesisitizwa pia kuhakikisha wanajua mipango ya utekelezaji wa kwenye vituo vyao ikiwemo ukusanyaji wa mapato, kusimamia matumizi sahihi ya fedha za Umma, usimamizi wa miradi ya maendeleo pamoja na kutumia vizuri taarifa za wakaguzi kwa kufuata ushauri wao kama njia ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Katibu wa afya wa Manispaa hiyo, ameeleza kuwa Kamati zote za vituo zinawajibika kwa Bodi ya afya ya Halmashauri kwa kutoa taarifa za utekelezaji wa shughuli zao kwani ndio msimamizi Mkuu wa masuala ya afya kwa ngazi ya Manispaa
Manispaa ya Ubungo ina Jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 22 vya Serikali.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa