Bodi ya Afya ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo leo imefanya kikao cha robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Kikao hicho kimefanyika hospitali ya Sinza kikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Ndg. Israel Sosthenes na Katibu wa Bodi ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Manispaa Dr. Peter Nsanya. pamoja na wajumbe wa bodi. Akiongea kwenye kikao hicho Mwenyekiti aliwaambia wajumbe kuwa kuna umuhimu wa bodi kutembelea miradi ya Afya ili kujionea hali halisi.
Mwenyekiti pia alisisitiza suala la ulinzi katika mradi wa Hospitali ya Wilaya. Alisema kuwa kuna haja ya kuhakikisha kuna ulinzi wa kutosha ili kudhibiti aina yoyote ya wizi au utoroshaji wa vifaa vya ujenzi unaoweza kujitokeza.
’’Niitake sasa idara ya Afya kuhakikisha maagizo yanayotolewa na bodi au Idara kwenda kwenye Zahanati na Vituo vya Afya yanakuwa kwenye maandishi” aliongeza Mwenyekiti.
Vile vile Mwenyekiti aliwaomba wajumbe kusisitiza wananchi kujiunga na Bima ya Afya ili waweze kupata matibabu na dawa kwa uhakika zaidi. Sambamba na hilo alimtaka Mganga Mkuu kuandaa mkakati wa kuelimisha wananchi juu ya faida za kujiunga na Bima ya Afya.
Ndg. Sosthenes pia alitilia mkazo suala la kuongeza mapato kwenye vituo vya Afya na zahanati, kusimamia na kutumia vizuri mapato yake katika kuboresha huduma kwa wananchi.
Nae Mganga Mkuu aliihakikishia bodi kuwa eneo ambalo hospitali ya Wilaya inajengwa ni salama na lina ulinzi wa kutosha.
Mganga Mkuu aliitarifu bodi kuwa kuanzia tarehe 14 hadi 28 mwezi huu Idara ya Afya itashirikiana na kanisa katoliki kutoa huduma za kibingwa katika kituo cha Afya Kimara, Zahanati ya Goba na Kituo cha Afya Mbezi. Baadhi ya vipimo vitakavyotolewa ni upimaji wa tezi dune na saratani ya shingo ya kizazi *’’HUDUMA HII ITAKUWA BURE NA ITAHUSISHA MADAKTARI BINGWA’’*
Mwenyekiti ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya *Mhe. Dr. John Pombe Magufuli* kwa ushirikiano wanaoutoa kwa miradi ya Afya na kuahidi kumpa Mhe. Rais ushirikiano.
Akifunga kikao Mwenyekiti aliwashukuru wajumbe kwa ushirikiano lakini alisisitiza kuwasimamia vizuri watumishi wa idara ya Afya vile vile kuhakikisha watumishi wanakuwa waadilifu na kujitolea kwa dhati ili wananchi wetu waweze kupata huduma bora.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa