Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kisare Matiko Makori amemaliza sintofahamu ya nani ni mmiliki halali wa eneo la zaidi ya ekari moja la Shule ya Sekondari Goba Mpakani iliyopo Kata ya Goba Mtaa wa Tegeta A.
Katika ziara yake hiyo Mkuu wa Wilaya aliambatana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo Ndg. James Mkumbo , Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Beatrice Dominic na wataalam kutoka Manispaa hiyo.
Kabla ya Mkuu wa Wilaya kutatua mgogoro huo alimtaka Kaimu Afisa Mipango miji wa Manispaa Ndg. Fadhili Hussein kutoa historia fupi ya eneo hilo.
Aidha Kaimu Afisa Mipango Miji wa Manispaa alisema kwamba eneo lote tayari wananchi wameshalipwa fidia na eneo ambalo limevamiwa lilikuwa linamilikiwa na Ndg. Ally Chande ambaye tayari alishalipwa Tsh. Milioni 314. Baada ya hapo mtu anayefahamika kama Kisoki alimuuzia eneo hilo hilo kitapeli mtu anayefahamika kwa jina la Kapama.
Aliongeza kuwa kuna makosa yalifanyika katika kupatiwa hati kwani Kapama ana hati ambayo aliipata kimakosa kwa kujua au kutokujua.
Baada ya maelezo hayo Mhe. Kisare alisema mambo matatu, Moja eneo sio la Kapama bali ni la Shule, Pili amepewa hati kwenye eneo ambalo tayari limeshafidiwa na Serikali. Tatu Kapama hatokaa aendeleze eneo hilo kwa sababu ni la Serikali.
Pia aliongeza kuwa kuna utaratibu wa kisheria ambao ulitumika kwenye utoaji wa hati na utaratibu huo huo utatumika kuona namna ya kufuta hati hiyo.
Sambamba na hayo aliwaomba wananchi kutoa taarifa kama eneo hilo litaendelezwa kwa namna yoyote kwani wao ndio wapo karibu na eneo hilo na tayari mhusika ameitwa mara kadhaa bila ya kuitikia wito huo na ana notisi ya kutoendeleza eneo.
Katika ziara hiyo wananchi walieleza kero wanazozipata kwenye maji, elimu, ulinzi na Usalama na mpaka wa Tegeta A na Kulangwa.
”Namuagiza Afisa Mipango Miji hadi kufikia Jumatano ya tarehe 22 mwezi huu mgogoro wa mpaka wa Mtaa wa Tegeta A na Kulangwa uwe umeisha kwani michoro ipo na pamoja na hilo ashughulikie mgogoro wa mpaka wa Matosa na Tegeta A.” aliongeza DC.
Katika suala la Ulinzi na Usalama DC alisema amesikia kilio cha wananchi kwa adha wanayoipata ya kufuata huduma mbali kutokana na kukosa kituo karibu na aliwachangia kiasi cha *Tsh. Milioni 1* kuendeleza ujenzi wa kituo.
Elimu, Mkuu wa Wilaya wa Wilaya alimuagiza pia Afisa Mipango Miji kuangalia kama eneo la Sekondari linatosha kujenga Shule ya Msingi ili Shule hiyo ijengwe kuwapungizia watoto kwenda mbali kwa ajili ya kupata elimu na kukutana na changamoto nyingi barabarani.
Wakati akifunga mkutano huo na wananchi Mkuu wa Wilaya alisisitiza suala la amani hasa wakati huu wa uchaguzi, vile vile wananchi wachague viongozi ambao watakuwa bega kwa bega kumsaidia Mhe. Rais Magufuli kuleta maendeleo na wanaokereketwa na kero zao na sio wanaowakimbia baada ya kuchaguliwa kama walivyofanya wengine wa upinzani.
”Niwaombe wajasiriamali wadogo mkachukue vitambulisho vya wajasiriamali ili mfanye biashara popote pale bila kubugudhiwa” Alisisitiza Mkuu wa Wilaya.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa