Leo tarehe 08/06/2022 Manispaa ya Ubungo imefanya mafunzo ya elimu ya lishe kwa walimu wakuu wa shule ya msingi na sekondari zilizopo Ubungo lengo ikiwa ni kuwajengea uelewa juu ya elimu ya lishe katika shule zao.
Akiongea Mratibu wa Lishe Manispaa ya Ubungo Beatrice Mossile ameelezea umuhimu wa Elimu ya Lishe mashuleni na kusisitiza juhudi za kuhakikisha watoto wanaelewa umuhimu wa Lishe kwa kuwa mabalozi wazuri kwenye jamii na hivyo kusaidia kuwa na jamii yenye kuzingatia mlo kamili na hivyo kuwa na lishe bora.
Aidha, Mossile ameelezea mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe na huduma za lishe kwa watoto chini ya miaka mitano shuleni ambapo amesema kuwa kwa sasa Serikali imekuja na mkakati wa huduma ya mkoba.
Ambapo watoto walioanza chekechea watapatiwa vitabu maalum vya kujazia taarifa zao za kliniki wakiwa shule pindi muda wa siku ya kliniki utakapofika lengo ni kuhakikisha watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano wanapata fursa ya huduma za kliniki pindi wawapo shuleni.
Sambamba na hayo Mossile ameelezea vifaa viitwavyo MUAC ambavyo vinafanya kazi yakupima lishe kwa wanafunzi kutegemeana na umri wao, ambapo walimu hao wameelezwa namna ambavyo wataalamu wa afya watatumia vifaa hivyo katika kupima lishe kwa wanafunzi.
Kwa upande wake mwakilishi wa Taasisi ya lishe Tanzania “NCT - Nutritition Connect Tanzania Ndugu Jackline Kawiche ameelezea madhara yatokanayo na lishe duni ikiwemo udumavu, upungufu wa damu, upungufu wa vitamini A, utapiamlo mkali, uzito pungufu na uzito uliokithiri.
Pamoja na hayo ameelezea madhara ya lishe kwa wanafunzi ikiwemo kiwango hafifu cha ufaulu, kutumia muda mrefu kufundisha, watoto kushindwa kuhudhuria masomo kila siku na magonjwa.
Kawiche amewaeleza walimu hao umuhimu wa kuwa na klabu za lishe mashuleni, Kuwa na kalenda ya Siku muhimu za Lishe, kuwa na bustani shuleni, kutenga muda wakutosha kwa wanafunzi na walimu mashuleni kushiriki michezo kwani kwa kufanya hayo yote yatapelekea kuimarisha Lishe bora kwa wanafunzi hao na kwa vizazi vijavyo.
#UbungoYetuFahariYetu
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa