Afisa Biashara wa Manispaa ya Ubungo Prisca Mjema wakati akitoa ufafanuzi kuhusiana na bei iliyowekwa na Manispaa kama malipo ya kodi ya vibanda vya soko la Shekilango na Sinza.
Akiongea na waandishi wa habari Afisa Biashara alisema kuwa Manispaa imekuwa ikipoteza mapato mengi katika vibanda vya masoko hayo kwa kukusanya mapato kidogo kulinganisha na hali halisi ya maeneo yaliyopo.
Aliongeza kuwa bei iliyopangwa ya Tshs.150,000 imewekwa kwa mujibu wa sheria ndogo ndogo za Halmashauri na vile vile imezingatia bei halisi ya upangishaji katika maeneo husika.
"Niwaombe wafanyabiashara wawe waelewa na kama kuna jambo hawajalielewa basi ofisi zetu zipo wazi kwa ajili ya kutoa ufafanuzi na Kama watalipa kodi kwa majibu wa mkataba basi Manispaa itaongeza mapato na kuweza kujenga miundombinu mizuri katika masoko yetu, kujenga masoko mapya, kujenga madarasa na maendeleo mengine". Alifafanua Afisa Biashara.
Nae Meneja Masoko wa Manispaa *Ndg. Geofrey Mbwama* alisema kwa soko la Shekilango lina jumla ya vibanda 293 na wanaolipa kodi ni vibanda 27 tu, soko la Sinza lina vibanda 192 na wanaolipa kodi ni vibanda 97 tu hali ambayo inapelekea Manispaa kupoteza mapato mengi.
Aliongeza kuwa katika vibanda hivyo wajenzi wengi wamevipangisha kwa wafanyabiashara wengine kinyume na sheria lakin pia wamekuwa wakiwatoza kodi kuanzia Tshs 80,000 hadi Tshs.600,000 kwa mwezi wakati Manispaa ikipokea 15,000 tu.
Aidha kwa utafiti na mazungumzo yaliyofanyika kati ya Manispaa na waliojenga vibanda mambo kadhaa yalibainika, Wajenzi wengi walikuwa hawana nyaraka wala gharama halisi, Wajenzi wote hawana mikataba kutoka Manispaa ya Ubungo, Hakuna ramani za wajenzi wa vibanda, waliojenga sio wanaofanya biashara bali wengi wao wamewapangisha watu wengine kinyume cha sheria na taratibu.
Mwisho Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Beatrice Dominic aliwaasa wamiliki wa vibanda hivyo kuweza kukubaliana na kulipa kiasi kilichopangwa kwa mujibu wa sheria kwa maendeleo ya wanaubungo na watanzania kwa ujumla katika kuleta maendeleo.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa