Wajumbe wa Kamati ya Kuthibiti UKIMWI Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo wamepatiwa mafunzo elekezi ya namna ya kutekeleza majukumu yao katika kufikia dira ya Taifa ya kutokomeza kabisa maambukizi ya virusi vya UKIMWI ifikapo mwaka 2030
Katika mafunzo hayo, wajumbe wameelezwa kuwa moja ya jukumu la kamati hiyo ni kutoa Elimu sahihi ya VVU na UKIMWI inayoendana na mazingira ya vihatarishi kwa makundi mbalimbali ikiwemo vijana, wanawake, wanaofanya biashara ya ngono na madereva wa vyombo vya moto kwani ndiyo yako kwenye hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu.
Akiongea baada ya mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Naibu Meya wa Manispaa Mhe. Hassan Mwasha amesema kuwa uundwaji wa Kamati za kudhibiti UKIMWI ngazi ya Kata na Mtaa ni moja ya mkakati mzuri katika kuhakisha suala ya mapambano dhidi ya UKIMWI yanafanyika hadi ngazi ya jamii.
Mwasha ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa kutekeleza majukumu yao ya kusimamia shughuli zote za mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI katika maeneo yao ili kufikia lengo la kumaliza kabisa janga hili linaloathiri Jamii hususani Vijana ambao ndio nguvu kazi ya Jamii na Taifa.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya UKIMWI katika Halmashauri ya Ubungo, Mratibu wa UKIMWI katika Manispaa hiyo Mercy Ndekeno amesema kuwa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kwa Manispaa ya Ubungo yamepungua kutoka 3.0 kwa mwaka 2020 na kufikia 2.3 kwa mwaka 2021 huku kundi la vijana likiwa kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi.
Ndekeno amesisitiza jamii kutowanyanyapaa watu wenye maambukizi badala yake waoneshwe upendo na kuwapa ushirikiano kwa kuhakikisha wanatumia vizuri dawa ili waendelee kufurahia maisha kama watu wasio na maambukizi.
Kuacha ngono zembe na Kupima afya ni hatua muhimu katika kupambana na maambukizi ya VVU na UKIMWI, kila mmoja achukue tahadhari.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa