Kamati ya siasa Wilaya ya Ubungo imefanya ziara yake kukagua miradi ya maendeleo katika Wilaya hiyo tarehe 19/06/2020.
Katika ziara hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Chama Wilaya ya Ubungo Ndg.Lucas Mgonja, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe.Kisare Makori, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Beatrice Dominic na kuhudhuriwa na Katibu tawala wa Wilaya ya Ubungo Ndg.James Mkumbo na viongozi mbalimbali wa chama cha Mapinduzi, Vyama rafiki vya upinzani na Wataalam kutoka Manispaa ya Ubungo.
Katika ziara hiyo Miradi iliyotembelewa ni Mradi wa ujenzi wa barabara ya Shekilango, Mradi wa ujenzi wa kingo za mto Ng'ombe kilomita 8.5 na Mto kiboko kilomita 3.5, Mradi wa ujenzi wa daraja la juu Ubungo (Flyover), Mradi wa ujenzi wa mabanda 7 ya wajasiriamali Mbezi luis uliopo Kata ya Mbezi na Mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Amani iliyopo Kwembe na dhumuni kuu likiwa ni kuona maendeleo ya miradi hiyo.
Aidha viongozi wa Chama Wilaya walipongeza juhudi ambazo zimefanywa na Wataalam waliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo kwa usimamizi mzuri wa miradi.
"Napenda kumshukuru raisi wetu wa awamu ya tano Dr.John Pombe Magufuli kwa maendeleo ambayo amefanya katika Wilaya yetu ya Ubungo na Tanzania kwa ujumla kwa kuboresha maendeleo ya wananchi wote" Alisema Mkuu wa Wilaya.
Sambamba na hilo Mkuu wa Wilaya alivishukuru vyama rafiki vya upinzani kwa heshima waliyoitoa na kuungana na uongozi wa Wilaya na Kamati ya siasa CCM ya Wilaya.
Pia Mkuu wa Wilaya aliwahakikishia wajumbe kuwa miradi ambayo walishindwa kufika imeakisi miradi ambayo imetembelewa.
Nae Mwenyekiti wa ACT wazalendo Wilaya kwa niaba ya vyama vingine aliushukuru uongozi wa Wilaya ya Ubungo ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya kwa ushirikishwaji wao.
"Niseme wazi Wilaya ya Ubungo ni Wilaya ya kuigwa kwani ndio ya kwanza kushiriki kwenye ziara ya kutembelea miradi na vyama vingine." Alisisitiza Mwenyekiti wa ACT
Aliongeza kwamba vyama vya upinzani vipo tayari kushirikiana na vyama vingine kwa maslahi ya Taifa.
Wakati akifunga Mwenyekiti wa CCM Wilaya alimpongeza Mkuu wa Wilaya na Wakuu wa Idara kwa kazi nzuri wanayoifanya kutekeleza miradi.
"Niwaombe wakati wa kupiga kura kumchagua Rais wote tukampigie kura John Pombe Magufuli kwa maendeleo ya Taifa letu na kwa kuzingatia Rais wetu kila siku anasisitiza maendeleo hayana chama."
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa