Manispaa ya Ubungo kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu Rais Idara ya Mazingira inatarajia kuanzisha mradi wa ujenzi wa vituo viwili vya kuchambua taka lengo ikiwa ni kuhamasisha matumizi ya mbinu bora na rafiki kwa mazingira katika usimamizi wa taka zinazozalishwa katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya uanzishwaji wa mradi huo, Dkt. Hussein Mohamed Omar kutoka ofisi ya Ofisi ya Makamu wa Rais Idara ya Mazingira, ameeleza kuwa mradi huo utagharimu dolla za kimarekani 102,500 huku manispaa ikiwajibika kutoa eneo la kutekeleza mradi huo.
Dkt. Omar amefafanua kuwa mradi huo utapunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana na kemikali sumu aina ya uPOPs zinazodumu kwenye mazingira kwa muda mrefu kutoakana na uchomaji taka.
“Vituo vitakavyojengwa vitakuwa vya aina mbili moja kituo kichafu yaani kinachopokea taka zisizotenganishwa na kituo kisafi ambacho kitapokea taka zilizochambuliwa” alieleza Dkt Omar.
Mradi huu unatarajia kuanza kutekelezwa mapema mwezi julai mwaka huu mara baada ya mkataba wa makubaliano kusainiwa kwa pande zote mbili.
Dkt. Omar ameendelea kueleza kuwa, maeneo 29 katika Manispaa ya Ubungo uchomaji wa taka ni miongoni mwa njia kuu za utupaji taka wakati Asilimia17% ya Taka zinazozalishwa huchomwa au kufukiwa ndio maana ubungo imepata fursa ya kuwa sehemu ya majaribio ya kutekeleza mradi huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mansipaa hiyo Beatrice Dominic amesema kuwa, Manispaa imeupokea mradi kwa mikono miwili kwani uhitaji wa vituo vya ukusanyaji, upembuaji na uchakataji wa taka ni muhimu sana katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, kuzalisha ajira pamoja na kupunguza sumu inayotokana na taka hizo.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa