Manispaa ya Ubungo imetoa mafunzo ya uhamishaji wa bima ya iCHF kwa watoa huduma ngazi ya jamii leo tarehe 11/03/2022 lengo ikiwa ni kuwajengea uelewa wa na namna ya kutumia mfumo wa uandikishaji wa bima hiyo.
Akiongea kwenye mafunzo hayo,Mratibu wa iCHF katika Manispaa hiyo Leticia Meena ameeleza kuwa iCHF ni bima iliyoboreshwa ambayo utaratibu wa kukata bima hiyo kwa kaya ya watu sita ni Tsh 150,000/= na Tsh 40,000/= kwa mtu mmoja na maelezo ya malipo ya watoa huduma hao yanakuwa Tsh 2,000/= kwa uandikishaji wa mtu mmoja na Tsh 7,500/= kwa uandikishaji wa kaya.
Meena ameeleza kuwa bima hii kwa sasa inatumika kwa hospitali zote za serikali kuanzia zahanati, kituo cha afya na hospitali za rufaa za Mikoa kwa utaratibu wa rufaa lakini kwa sasa mteja wa bima hizi anaweza kuanzia kituo cha afya moja kwa moja.
Aidha, Meena amewataka watoa huduma hao kutumia sehemu zenye mikusanyiko ya watu popote watakapo pata fursa ya kufanya hivyo kwa ajili ya kwenda kuhamasisha wananchi kukata bima hiyo kwani mpango wa serikali ni kuona kila mwananchi anakuwa na uhakika wa matibabu.
“Tujifunze kuwekeza kwenye Afya kwa kuwa na uhakika wa matibabu kwa kukata bima ya iCHF.” Alisema Meena.
Kwa upande wake Afisa Tehama anaesimamia mfumo wa uandikishaji wa wateja wa bima hiyo Victoria Kazuzuru ameeleza kuwa huduma zinazotolewa kwenye bima hiyo ni huduma zote ambazo zinapatikana kwenye zahanati, kituo cha afya na hospitali zote za rufaa za Mkoa ikiwemo upasuaji mkubwa na mdogo, kulazwa, macho, kumuona daktari, matibabu ya awali ya figo na moyo, tezi dume na magonjwa mengine
“Bima hii inapaswa kuhudumiwa sawa na bima nyingine na asitokee daktari yeyote atakae mzuia mteja wa bima hii kupata huduma yeyote ambayo inatolea zahanati, kituo cha afya au hospitali yeyote ya rufaa na kwamba ikitokea dawa zimeisha basi daktari anapaswa kumwelekeza mgonjwa zahanati au kituo cha afya au hospitali ili mgonjwa apate huduma sahihi.” Alisema Kazuzuru.
Kazuzuru amesema kuwa watoa huduma hao wanapaswa kuwa na simu janja ambazo zitawekewa mfumo kwa ajili ya kuandikishia wateja wa bima hiyo.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa