Manispaa ya Ubungo imeanza maadhimisho ya wiki ya utumishi wa Umma kwa kuwatembelea na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Manispaa hiyo ikiwemo kuhakikisha wanapata maslahi yao kwa wakati.
Akiongea na watumishi wa Manispaa hiyo wakati alipowatembelea kwenye vituo vyao vya kazi, Afisa utumishi wa Manispaa hiyo Selemani Kateti ameeleza kuwa Manispaa kupitia idara yake inajitahidi kushughulikia maslahi ya watumishi ikiwemo upandishwaji wa madaraja, malimbikizo ya mishahara pamoja na gharama za likizo.
Kateti amefafanua kuwa "Kwa zoezi linaloendelea la upandishaji madaraja ya watumishi, Manispaa ya Ubungo inatarajia kupandisha madaraja watumishi 1409 ambao Kati ya hao walimu 1090 watapandishwa, watumishi wa idara ya afya 206 na watumishi wengine 113"
Aidha, Kateti amewaeleza watumishi hao kuwa wakati Serikali inatekeleza wajibu wake wa kutatua changamoto zao watambue kuwa wajibu wao ni kufanya kazi kwa uadilifu na weledi mkubwa katika kuwatumikia wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kutokana na namna Manispaa inavyoshughulikia maslahi ya watumishi wa Manispaa hiyo, baadhi ya watumishi wameishukuru Serikali kwa kushughulikia changamoto zao hasa upandishwaji wa madaraja na wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, ueledi na bidii kubwa katika kufikia maendeleo ya Taifa kupitia utumishi wao
"Nimefurahi leo kutembelewa na Afisa utumishi katika kituo chetu cha kazi Kwa lengo la kusikiliza kero zetu na kuzitoolea majibu hapo hapo, mfano amehakikisha wote tunaotakiwa kupanda katika kituo chetu tupo kwenye orodha na ambao hawakuwa wamewasilisha nyaraka zote amehakikisha nyaraka hizo wanawasilisha ili nao wapate haki ya Kupanda, tunamshukuru Sana"
Maadhimisho ya wiki ya utumishi wa Umma Kwa mwaka huu yameeanza leo Juni 16 na yatamalizika Juni 23 yakiongozwa na Kauli mbiu isemayo *Kujenga Afrika tunayoitaka kupitia utamaduni wa uadilifu ambao utastawisha Uongozi wenye maono hata katika mazingira ya Migogoro*
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa