HALMASHAURI ya Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es salaam leo tarehe 3 oktoba, 2020 imekabidhiwa mradi wa ujenzi wa jengo jipya la utawala linalojengwa katika kata ya Kwembe Mtaa wa mji mpya na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wenye thamani ya shilingi bilioni 6.2 baada ya kuvunja mkataba wa ujenzi Wa mradi huo tarehe 23 septemba mwaka huu kutokana na kushindwa kukamilisha kwa wakati mradi huo.
Maamuzi hayo yamefikiwa leo tarehe 3 oktoba, 2020 kwenye kikao cha pamoja kati ya wakala wa majengo Tanzania (TBA) na timu ya menejimenti ya manispaa ya Ubungo kilichomtaka TBA kukabidhi mradi huo kwa Manispaa ili atafutwe mkandarasi mwingine wa kumalizia kazi zilizobaki.
Halmashauri imefikia hatua ya kutaka kukabidhiwa mradi huo baada ya mkandarasi huyo kushindwa kukamilisha mradi kwa mujibu wa mkataba ambapo mradi huo ulipaswa kukamilika na kukabidhiwa januari 2020 tangu uliposainiwa desemba 2018, lakini hata baada ya kuongezewa muda wa zaidi ya miezi sita alishindwa kukamilisha mradi.
Akiongea kwenye kikao hicho Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Bibi Beatrice Dominic alisema kuwa baada ya kuongezewa muda wa kukamilisha mradi TBA walipaswa kukabidhi mradi tarehe 19 septemba, 2020 lakini bado hawakuwa wamemaliza kazi ndio maana Manispaa iliamua kuvunja mkataba na leo mkandarasi "tunamtaka atukabidhi mradi ili tutafute mkandarasi mwingine wa kukamilisha mradi"
Beatrice amefafanua kuwa “ifahamike kuwa Halmashauri imeendelea kulipa kodi ya majengo ya ofisi yaliyopangwa katika maeneo tofauti jambo ambalo ni kinyume na maagizo ya serikali”
Aidha, Beatrice ameendelea kueleza adha wanayopata wananchi wakati wa kupata huduma mbalimbali kwani ofisi zimetawanyika katika maeneo tofauti “ndio maana tulifika maamuzi ya kuvunja mkataba na TBA na leo tumemtaka atukabidhi mradi kwani ameshindwa kutekeleza mradi kwa wakati"
Serikali iliamua kutoa fedha za ujenzi wa jengo hili ili kusogeza huduma karibu na wananchi, kucheleweshwa kwa maradi huu ni kwenda kinyume na agizo la serikali linalozitaka Halmashauri zote nchini kuwa katika maeneo yake ya utawala. Hadi kufikia sasa mradi umefikia asilimia 80
Kwa upande wao TBA wamekubaliana na uamuzi wa kukabidhi mradi kwa Halmashauri itafute mkandarasi mwingine kumalizia kazi zilizobaki
Aidha Timu ya wataalamu imeundwa ili kufanya tathimini ya kazi zilizobaki kwa pamoja ili kutenda haki kwa kila upande
Watalaam kutoka wakala wa majengo Tanzania (TBA) na Manispaa ya Ubungo wakikagua mradi wa ujenzi wa jengo la Utawala lililiokuwa linajengwa na TBA kabla ya kuvunjiwa mkataba leo tarehe 3 oktoba, 2020 katika ukumbi wa jengo hilo
IMEANDALIWA NA;
Kitengo cha habari na uhususiano
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa