Shirika la OCODE TANZANIA limekabidhi chumba kimoja cha darasa la mfano kwa ajili ya wanafunzi wa awali, viti 16, meza Tatu na zana za kufundishia vyenye thamani ya shilingi milioni 39 katika Shule ya msingi Kiluvya iliyopo Kata ya Kibamba Manispaa ya Ubungo lengo ikiwa ni kuhamasisha wanafunzi kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Akiongea katika hafla hiyo ya kukabidhi miundombinu hiyo Mkurugenzi wa OCODE Bw. Joseph Jackson amesema sambamba na ujenzi huo wamefanikiwa kutoa mafunzo ya mbinu na zana mbadala za kufundishia iitwayo jifunze kwa walimu wa darasa la awali, la kwanza, la pili na la tatu ili kuwezesha wanafunzi kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Joseph ameeleza kuwa mbinu hiyo imesaidia wanafunzi wengi kujua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa muda mfupi na ametoa wito kwa Manispaa kuendeleza mbinu hiyo.
Aidha, ameeleza kuwa zoezi hilo la ugawaji wa vitu hivyo limeambatana na kauli mbiu isemayo “ulinzi na usalama wa watoto ni jukumu letu sote tupaze sauti kupinga ukatili dhidi ya watoto wetu sote”
Joseph ameendelea kueleza kuwa kwa muda wa Miaka minne mfululizo imekuwa ikishirikiana na manispaa hiyo kwa kujenga shule za awali katika Shule ya msingi Kibwegere, Malamba Mawili, Goba na Kiluvya kwa gharama za Shilingi milioni 113.3.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kheri James amelipongeza Shirika hilo na kutoa wito kwa wadau wengine kuendelea kuisaidia jamii kama ambavyo wamefanya OCODE.
Kheri ameitaka jamii kutofumbia macho ukatili wa watoto kwani ukatili huo usipodhibitiwa juu ya watoto wetu wataendelea kunyanyasika. Pamoja na changamoto za maisha zilizopo ni lazima kutenga muda kwa watoto wetu.
“Mapambano dhidi ya ukatili wa watoto ni wajibu wa kila mmoja wetu” Alisema James
Nae Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bi. Leah Linus Sanga ameeleza Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 2,109 na jumla ya vyumba vya madarasa 11 ya msingi na darasa 1 la awali kutokana na wanafunzi waliopo kuna uhitaji wa vyumba 13 vya madarasa.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa