Manispaa ya Ubungo jijini Dar Es salaam leo januari 7 2020 imetoa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya shilingi bilioni 1.1 kwa vikundi 111 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa ajili kuendeleza na kukuza mitaji ya biashara zao na hatimaye kujikwamua na umasikini.
Mikopo hiyo iliyotolewa leo baada ya kupata mafunzo ya namna ya kuendesha biashara zao kwa vikundi hivyo vyenye wanufaika 1566 ambapo vikundi vya wanawake 62 vitapata shilingi milioni 560,135,200, milioni 424 161,000 kwa vikundi 38 vya vijana na milioni 119 , 000, 000 kwa ajili ya vikundi 11 vya watu wenye ulemavu.
Wanufaika wa mikopo wakifuatilia mafunzo kabla ya kukabidhiwa mikopo
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo na kutoa hundi ya mikopo kwa vikundi hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare Makori amewaeleza wajasiliamali hao kuwa utoaji wa mikopo hiyo ni utekelezaji wa sera ya serikali inayozitaka Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwezesha wananchi kiuchumi na kuondokana na umasikini
Makori amesema kuwa "Nawapongeza kwa kukidhi vigezo na kupata mikopo hii, nawasii mkaitumie mikopo hii kwa ajili ya kukuza biashara zenu na sio kununua vijora vya sherehe kwani serikali imeamuankutoa mikopo hii isiyo na riba ili ujasiriamali uwe njia ya kumkwamua mwananchi kiuchumi kwa kukuza mitaji yao"
Makori ameendelea kueleza kuwa utoaji wa mikopo hiyo unaenda sambamba na kufanya marejesho kwa wakati ili kuongeza fursa kwa watu wengine kupata mikopo lakini pia kuongeza kiwango cha kukopesha " hivyo rejesheni mikopo kwa wakati"
"Tusififishe ndoto na nia njema ya serikali ya kukuza uchumi wa wananchi kwa kutorejesha, hengeni nidhamu na uaminifu kwenye marejesho ili tupanue wigo wa kukopesha watu wengi zaidi na kutengeneza mabilioni" amesisitiza Makori
Kwa upande wake mratibu wa mfuko wa wanawake vijana na walemavu wa manispaa hiyo Elizabeth Kebwe ameeleza kuwa vikundi vinavyopata mkopo awamu hii vinajishughulisha na shughuli za kilimo, mifugo, uzalishaji mali, usindikaji wa bidhaa mbalimbali, viwanda vidogovidogo ambavyo vimekidhi vigezo wa kupata mkopo.
Kebwe amesema kuwa kwa kipindi cha miaka 3 kuanzia mwaka 2017 hadi 2019, Manispaa imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi 3,966,405,785 kwa vikundi 914 yenye wanufaika 9281 na kati ya fedha hizo shilingi 1,031,003, 687.25 ndio zimerejeshwa.
Aidha Elizabeth kebwe amefafanua kuwa mikopo inayotolewa leo kuna vikundi vitapata mkopo wa milioni 70 kikiwa ndicho kiwango cha juu kuwahi kutolewa na Manispaa kwa vikundi vya wajasiriamali "haya ni mafanikio makubwa sana kwa Manispaa na wajasiliamali kwani dhana ya mikopo hii ni kukukuza uchumi.
Pamoja na kutoa fedha kwa vikundi lakini pia Manispaa imefanikiwa kutoa bajaji 45, pikipiki 22 na toyo 1 vikundi vya vijana na walemavu "tunaimani vyombo hivi vya usafiri vitaanza kuwaingizia kipato, nawasii muanze marejesho haraka zaidi" alisisitiza Kebwe.
Akiongea kwa niaba ya wajasiriamali wenzake stuwart Simon banda kutoka kikundi cha jiwezeshe Goba ameishukuru serikali na Manispaa ya ubungo kwa kutoa mikopo kwa wajasiriamali ili kukuza mitaji ya biashara zetu zitakazotusaidia kujikwamua kiuchumi.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa