Manispaa ya Ubungo imezindua kampeni ya masuala ya ulipaji wa ushuru, leseni, tozo, kodi na ada mbalimbali, kampeni ambayo itafanyika kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia tarehe 05/05/2022 hadi tarehe 05/06/2022 ambayo itafanyika kupitia mitandao ya kijamii (Instagram, Facebook, Twitter, Youtube na Clubhouse) yenye jina la ‘ubungomanispaa’ lengo kubwa ikiwa ni kujenga uelewa na umuhimu juu ya ulipaji kodi, ada, ushuru na tozo mbalimbali za Manispaa.
Akifanunua katika kampeni hiyo Afisa Habari wa Manispaa hiyo ndugu Joina Nzali amesema Manispaa imeamua kuanzisha kampeni hii kwa njia ya mitandao ya kijamii ili kutoa fursa kwa wananchi na wafanyabiashara kushiriki kikamilifu kwa kupata elimu, kuuliza maswali, kufanya mijadala na kupata ufafanuzi wake, kutoa ushauri na kuhamasisha jamii kwa ujumla kuhusu ulipaji wa kodi mbalimbali za Manispaa.
Aidha, Nzali amewataka wananchi na wafanyabiashara wote kushiriki kwenye kampeni hii kwa kufatilia katika mitandao ya kijamii (instagram, twitter, Clubhouse na youtube) kwa jina la Ubungo Manispaa ili kupata nafasi nzuri ya kujenga uelewa wa pamoja juu ya kampeni hii kati ya serikali na wafanyabiashara kwa maeneo mbalimbali ndani ya Manispaa ya Ubungo.
Kwa upande wake Afisa biashara wa Manispaa hiyo ndugu Peter Ngoti ameeleza kuwa ada, tozo, ushuru na kodi ni moja ya vyanzo vya mapato ya Manispaa ambapo wananchi ndio wachangiaji wakubwa wa mapato hayo kutokana na biashara zao na hivyo kusaidia Manispaa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo shule, vituo vya afya miundombinu ya barabara na nyinginezo.
Aidha Ngoti ametoa elimu kwa wananchi juu ya ufahamu na ulipaji wa mapato na kuwasihi kuacha kusikiliza taarifa zisizo rasmi juu ya ulipaji wa mapato kutoka kwa wapotoshaji wa mitaani (vishoka).
Akiongea Mgeni rasmi wa uzinduzi huo Ndugu Zacharia Kimaro ambae ni meneja wa kampuni ya Musa Investiment automotive amesema anaipongeza Manispaa kwa kampeni hii ambayo italeta tija kwa wafanyabiashara endapo watachangia mapato kwani kwa kufanya hivyo watakuwa huru katika kufanya biashara zao ikiwa ni pamoja na kupata fursa mbalimbali na amewataka wafanya biashara wote kulipa mapato yote ya Manispaa kwa hiari kwani kwa kufanya hivyo Manispaa itaweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa