Kuelekea siku ya Maadhimisho ya magonjwa yasiyoambukiza, Manispaa ya Ubungo kwa kushirikiana na vikundi Mbalimbali vya jogging katika Manispaa hiyo, imefanya mazoezi ya kukimbia (jogging) lengo ikiwa ni kuhamasisha jamii kufanya mazoezi kama njia bora ya kuepuka magonjwa hayo.
Mazoezi hayo yaliyoongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo ndugu James Mkumbo yalianzia Hospitali ya Wilaya iliyopo Kimara Baruti hadi Daraja la Kijazi ( kijazi Interchange)
Akiongea baada ya mazoezi hayo, Mkumbo aliwaeleza wananchi kuwa mazoezi ni afya hivyo kila mtu anapaswa kufanya ili kuimarisha afya yake na hivyo kuepuka magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya akili,figo, pumu, saratani na magonjwa ya moyo.
“Mazoezi ni afya ni vema tukajenga utaratibu wa kufanya mazoezi ili kuweka miili yetu kuwa imara na hivyo kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanasababiswa na ulaji usiozingatia lishe bora na kutofanya mazoezi” alieleza Mkumbo.
Kwa upande wake Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Kimara Ismail Mvungi alisema aliamua kuvishirikisha vikundi vya jogging kushiriki mazoezi hayo na kuwaeleza wananchi wa Kimara na Ubungo juu ya ufunguzi wa Hospitali ya Wilaya inayotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni hivyo ni vyema kuandaa mazingira mazuri ya hospitali hiyo ambapo wananchi waliojitokeza kwenye mazoezi hayo walishiriki kupanda miti kwa ajili ya kutunza mazingira na kuchangia damu chupa 24 ikiwa ni maandalizi ya ufunguzi wa Hospitali hiyo
Mheshimiwa Diwani wa kata ya kimara Ismail Mvungi akichangiaji damu leo oktoba 30,2021 katika hospitali ya Wilaya
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mansipaa ya Ubungo Dr. Peter Nsanya amesema kuwa wananchi wamehamasishwa na kuchanja kwa hiari chanjo ya UVIKO 19 kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo.
Akiongea kwa niaba ya vikundi vya jogging vilivyoshirki katika mazoezi hayo, Mustapha Hamisi ameipongeza serikali kwa kuwashirikisha katika kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi lakini pia kushiriki katika kuchangia damu ikiwa ni maandalizi ya kuifungua hospitali ya Wilaya ambayo ilisubiriwa kwa muda mrefu.
Hamisi amesema “Nawasii wananchi hususani vijana kujiunga na vikundi vya jogging vilivyopo kwenye maeneo yao kwa ajili ya kuimarisha afya za miili yao hali itakayowasaidia kutopata magonjwa yanayosababishwa na unene uliopita kiasi”.
Maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasiyoambukiza yataanza tarehe 6 hadi 12 ya mwezi novemba ambapo Manispaa ya Ubungo itaadhimisha kilele cha siku hiyo tarehe 12 novemba, 2021.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa