Mbunge wa Jimbo la Ubungo Profesa Kitila Mkumbo amewapa motisha walimu wa Sekondari waliofaulisha somo la Hisabati kwa daraja A kwenye matokeo ya wanafunzi wa kidato cha nne jimboni humo ambapo ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa mwezi Aprili 2021 ikiwa ni mkakati wa kuongeza ufaulu wa somo hilo
Akifafanua ahadi hizo Profesa Mkumbo amesema, kila A moja mwalimu wa somo atapata Tsh 100,000, mwanafunzi aliyepata alama A atalipiwa Ada yote ya kidato cha tano na sita huku waliopata alama B watalipiwa nusu Ada pamoja na zawadi hizo amesema wanafunzi na walimu hao watapata fursa ya kwenda hifadhi ya Saadan kwa siku tatu .
Shule 6 zimefanikiwa kupata tuzo hizo ambazo ni Sekondari ya Urafiki imepata A moja, Mugabe imepata A moja, Mabibo imepata A tatu, Mburahati imepata A tatu, Makurumla imepata A nne na Kimara imepata A 18.
Akieleza mafanikio ya mkakati huo mbele ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ambae ndiye mgeni rasmi wa tukio hilo, wadau wa elimu, Madiwani, waalimu, wanafunzi na wazazi Profesa Mkumbo ameeleza kuwa mkakati huo umefanikiwa kwani ufaulu wa somo hilo umeongezeka kutoka 11.6% kwa matokeo ya mwaka 2020 hadi kufikia 16% kwa matokeo ya mwaka 2021
"Mkakati huu umefanikiwa kwa sababu kwa matokeo ya mwaka 2020 hakukuwa na mwanafunzi aliyepata alama A lakini baada ya mkakati huu wa kuamua kuwapa motisha walimu, wanafunzi 30 wamepata daraja A na wanafunzi 31 wamepata daraja B kwa matokea ya mwaka 2021 wakati kwa matokeo ya mwaka 2020 wanafunzi 9 tu walifaulu kwa alama B pekee".
Profesa Mkumbo ameendelea kufafanua kuwa hakuna elimu bila mwalimu hivyo kumpa motisha mwalimu kunachochea kiu ya kufundisha ambapo matokeo yake yanaongeza ufaulu kwa kiasi kikubwa
Kwa upande wake Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amempongeza Profesa Kitila Mkumbo kwa mkakati wake uliozaa matunda ya kuongeza ufaulu somo hilo kwa kuwapa motisha walimu na kwamba serikali imebeba mkakati huo na itatoa ushirikiano katika kufanya utafiti wa kuongeza ufaulu wa somo hilo unaotarajiwa kufanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa