Mhe. Mbunge wa Jimbo la Ubungo ambaye pia ni Waziri wa Ofisi ya Rais Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo leo tarehe 4 januari, 2021, amefanya kikao na watumishi wa Manispaa ya Ubungo kilicholenga kujua majukumu ya kila idara na vitengo na kuweka mikakati ya namna ya kutatua kero za wananchi katika sekta mbalimbali.
Akizungumza na watumishi hao Mhe. Mbunge amesema, amelazimika kufanya kikao hicho kupata uelewa wa utekelezajia wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na Idara pamoja na vitengo ili kufahamu mipango yao katika kuhudumia wananchi na changamoto zinazowakabili na hatimaye kuweka mikakati wa pamoja wa namna ya kuzitatua
Wakuu wa Idara na vitengo wa Manispaa ya Ubungo wakimsikiliza kwa makini Mbunge wa jimbo la ubungo prof Kitila Mkumbo (hayupo pichani) alieleza mikakati ya kuboresha utoaji huduma kwa wananchi
Prof Kitila ameeleza kuwa "Kikao hiki kitanipa fursa ya kujua mipango yenu na wapi mnakwama ili kwa nafasi yangu nione tunashirikianaje kupanga mikakati ambayo itasaidia kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo la ubungo kwa kutatua kero mbalimbali ikiwemo ubovu wa barabara za mitaa, elimu afya, maji na namna ya kutengeneza mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa sekta ambayo 50% ya wakazi wa jimbo hilo wanaitegemea"
Prof. Kitila ameendelea kuwaeleza watumishi hao kuwa hali ya barabara nyingi za mitaa ndani ya jimbo la Ubungo ni mbaya hazipitiki muda wote na ndio kero ya kwanza kwa wananchi hivyo " kama manispaa kwa kishirikiana na tarura tuone namna ya kuanzisha mfumo ambao utawezesha barabara za mitaa kufanyiwa matengenezo angalau kiwango cha changalawe ili ziweze kupitika muda kwani wananchi wanateseka sana"
Aidha prof Kitila ameendelea kueleza kuwa uboreshaji wa upatikanaji wa huduma za elimu, maji na afya utapapelekea kuitafsiri kwa vitendo ilani ya chama cha mapinduzi ambayo imejikita zaidi kutatua kero za wananchi katika nyanja zote " nyinyi kama wataalamu mnapaswa kubuni mbinu za kitaalamu zinazolenga kupuguza kero hizo ili kujenga uaminifu kwa serikali yao"
Baadhi ya watendaji wa kata za Jimbo la Ubungo wakiwa kwenye kikao
"Utoaji wa huduma bora unategemea upatikanaji wa fedha, hivyo tunapaswa kutengeneza mazingira mazuri ya kufanyia biashara ikiwemo kuimarisha masoko yaliyopo pamoja kusimamia kwa makini ukusanyaji wa mapato kwenye vyanzo vyote vilivyoainishwa kwenye bajeti" anaelekeza prof Kitila
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Beatrice Dominic ameeleza kuwa Manispaa imekuwa ikitoa fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, ujenzi wa madarasa, vituo vya kutolea huduma za afya na miundombinu mingine lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma mhimu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Beatrice Dominic akitoa ufafanuzi wa namna Manispaa inavyotekeleza shughuli mbalimbali kwenye kikao kati ya watumishi wa Manispaa hiyo na Mhe Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof Kitila Mkumbo.
"Kutokana na ongezeko la ufaulu wa wanafunzi wa kujiunga kidato cha kwanza, Manispaa imetoa milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 37 pamoja na madawati lengo ikiwa kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu hawapotezi nafasi ya kusoma kwa sababu ya ukosefu wa vyumba vya madarasa" ameeleza Beatrice
Akichangia hoja kwenye kikao hicho, Afisa Elimu Msingi wa Manispaa hiyo Abdul Buhety amempongeza Mhe. Mbunge kwa kufanya kikao hicho ambacho kimempa fursa ya kujua utekelezaji wa shughuli mbalimbali na kueleza mikakati ya pamoja ya namna ya kutatua kero mbalimbali kwa ustawi wa wananchi wa Jimbo hilo na Manispaa kwa ujumla.
Afisa Elimu Msingi wa Manispaa hiyo Abdul Buhety( aliyesimama) akichangia hoja kwenye kikao kati ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof Kitila Mkumbo na watumishi wa Manispaa hiyo leo tarehe 04.01.2021
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa