Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira,na Wenye ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ameadhimisha sikukuu ya Nanenane kwa kutembelea vikundi vya vijana vilivyopo Manispaa ya Ubungo ambavyo vimenufaika na mkopo wa 10% inayotokana na mapato ya ndani ya Manispaa hiyo ambapo amevipongeza vikundi hivyo kwa kutendea haki mikopo hiyo kwa kufanya uzalishaji wenye tija na kurejesha kwa wakati.
Katika ziara Mhe. Katambi ametembelea kikundi cha Umoja ni Nguvu kinachojihusisha na utengenezaji wa mapambo ya ndani kwa kutumia unga wa gypsum na kikundi cha BRIACO kinachojishughulisha na uzalishaji wa Kripsi za viazi mbatata na kueleza kuwa dhima ya Serikali ni kuona vijana wanajiajiri kwenye shughuli za uzalishaji wakisaidiwa na Halmashauri kwa kuongezewa mikopo isiyo na riba kama sheria inavyoelekeza.
Mhe. Katambi ametaka vijana kuwa na malengo, kusudio na shabaha katika mipango kazi yao ili waweze kuzalisha bidha zenye ushindani kwenye soko la ndani na nje, kujikwamua kiuchumi, kuzalisha ajira na kuanzisha viwanda kwa kutumia elimu na ujuzi waliyonao kwani vijana ndio nguvu kazi ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Kutokana na utendaji kazi mzuri wa vikundi alivyotembelea ikiwemo kufanya marejesho kwa wakati, Mhe. Katambi ameielekeza Manispaa ya Ubungo kuviongezea kiwango cha mkopo vikundi hivyo kwenye maombi yao mengine ili viweze kuboresha na kuongeza uzalishaji wa bidhaa zao.
Aidha Mhe. Katambi ameeleza kuwa “Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya mwaka 2012, vijana wanakadiriwa kuwa nusu ya idadi ya watu wote kwa maana hiyo ni kundi muhimu lenye maarifa, ujuzi na usomi,nguvu kazi kwa ujumla hivyo sisi kama serikali lazima tuwekeze nguvu katika kulisaidia kubadilisha mitazamo waliyonayo, kuwahudumia kulingana na mahitaji yao ili waweze kujitegemea na kufanya majukumu ya kimaendeleo”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Beatrice Dominic amevipongeza vikundi hivyo kwa kazi nzuri na kuahidi kuwaongezea nguvu ikiwemo kupata eneo la kudumu la kufanyia kazi, kutangaza bidhaa zao pamoja na kutumia bidhaa (mapambo zinazotengenezwa na unga wa gypsum) kwenye miradi ya Halmshauri.
Wakiongea kwa nyakati tofauti, wananvikundi wameshukuru kupata ugeni huo mkubwa na kuona kuwa wameheshimishwa na wameahidi kuendelea kufanya shughuli zao kwa weledi mkubwa ili kufikia malengo waliyojiwekea hususani kuwa wazalishaji wakubwa wa bidhaa hizo
Hadi kufikia Juni 2021/2022 Halmashauri ya Manispaa ya ubungo imekopesha jumla ya shilingi 7,559,514,415 kwa vikundi 1,350 vyenye wanufaika 10,163 ambapo kati ya vikundi hivyo vikundi vya wananwake ni 747 vimekopeshwa shilingi 3,834,437,630 vikundi vya vijana 537 vimekopeshwa shilingi 3, 190,926,785 na vikundi vya watu wenye ulemavu 66 vimekopesha shilingi 534,150,000.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa