Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam, imefanikiwa kuviwezesha vikundi vya wajasiriamali wadogo 222 kukuza uchumi kwa kutoa mikopo isiyo na riba yenye thamani ya shilingi 1,274,420,000/= kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa serikali wa kukuza uchumi kwa wananchi wake kupitia fedha za mapato ya ndani (10%)
Taarifa hiyo imetolewa na Afisa Maendeleo ya jamii wa Manispaa hiyo, Rose Mpeleta baada ya kutembelea baadhi ya vikundi vya wajasiriamali wadogo vilivyopewa mkopo na manispaa hiyo, na kueleza kwamba, Manispaa ina jumla ya vikundi 5418 vilivyosajiliwa lakini vikundi 222 ndivyo vilivyofanikiwa kupata mkopo.
Mpeleta ameseama kuwa vikundi vilivyopata mikopo vimefanikiwa kuboresha biashara zao kwa kuongeza mitaji pamoja na kuboresha Maisha yao na kuondokana na umasikini “hilo ndio lengo kuu la serikali kuhakikisha wananchi wanafikia uchumi wa kati kwa kujishughulisha na kazi za ujasiliamali ili kukuza kipato” .
Vikundi vina miradi mizuri ambayo inawaingizia kipato ikiwemo ufugaji, biashara za maduka, mama lishe, ujenzi, na mingine mingi na urejeshaji wake unakwenda vizuri kwani biashara zao zinaendelea vizuri.
Kikundi cha walemavu kilichopo kata ya kimara wakijadiliana kuhusu maendeleo ya kikundi. Kikundi kimepata mkopo wa shilingi milioni 5
Mwenyekiti wa kikundi cha wanawake cha HONDOHONDO MLEZI WA WANA kilichopo kata ya Kimara Manispaa ya Ubungo Sara Godwin ameleza kuwa kabla ya mkopo alikuwa na biashra ya genge dogo tu lakini baada ya kupata mkopo biashara yake imepanuka ambapo ameweza kuongeza duka pamoja na kuongeza bidhaa kwenye genge lake.
Mwenyekiti ameeleza kuwa “naishukuru Manispaa ya Ubungo na Serikali ya awamu ya tano kwa kutoa mikopo isiyo na riba kwani imetuongezea mitaji ya biashara zetu lakini pia Maisha yetu yamebadilika kwani tunauwezo wa kupata mahitaji ya msingi na kuweka akiba.
Aidha Sara ameiomba serikali kuongeza viwango vya mikopo hiyo ili wajasiliamali wakuze biashara zao na kwa kufanya hivyo tutakuwa kwenye maisha ya uchumi wa kati kwa vitendo.
Mathew Samson Swai ni moja ya wanakikundi cha vijana cha wajasiriamali cha Baruti Umoja Group, amewashauri vijana kujiunga kwenye vikundi kwani ni njia rahisi ya kufikia maendeleo, aidha Swai amewashauri vijana kuwa wavumilivu kwa wateja, kutokata tamaa pamoja na kujifanyia tathimini ya biashaya yake ili kujua kama biashara inakua au inashuka.
Kikundi cha Baruti umoja Group chenye wanachama 22, pamoja na kuwa na biashara ya mwanakikundi mmojammoja lakini pia kimefanikiwa kununua Bajaji 4 kutokana na mikopo ya ujasiriamali inayotolewa na manispaa ya Ubungo ambapo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 walipata mkopo wa shilingi milioni 25,500,000/= na wameanza kufanya marejesho.
Mikopo inayotolewa kwa vikundi vya wajasiriamali wadogo haina riba, vikundi vinarudisha kiasi kilekile cha fedha walichokopa, na urejeshwaji wake unafanyika baada ya miezi mitatu baada ya kupata mkopo.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa