Leo Desemba 28, 2022 Wageni kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mtwara wakiwemo Waheshimiwa madiwani na wataalamu wa Halmashauri hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mhe. Selemani Nampanye pamoja Mkurugenzi wa Halmashauri Ndugu Yerica Yegella wamefanya ziara ya mafunzo kwa kutembelea Manispaa ya Ubungo lengo ikiwa ni kujifunza juu ya ukusanyaji wa mapato na usimamiaji wa miradi ya Maendeleo.
Akiongea Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Dkt Peter Nsanya amewaeleza wageni hao namna Manispaa hiyo inasimamia ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi ambapo kila kata ina mlezi wake ambao ni wakuu wa idara na Vitengo na maafisa biashara ambao wamekuwa wakishirikiana na viongozi wa Kata wanazozilea katika kuhakikisha mapato yanakusanywa kwa usahihi na ufanisi.
Akitoa maelezo juu ya shughuli mbalimbali za Manispaa, Mchumi wa Manispaa ya Ubungo ndugu Grace Mwaigaga amesema kuwa Manispaa ya Ubungo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imekadiriwa kukusanya Bilioni 32 ambapo mpaka Desemba 25, 2022 imeshakusanya Bilioni 15 sawa na asilimia 48 za makusanyo. Aidha, Uwepo wa Kituo cha Magufuli umekuwa ni chachu ya kuongeza mapato kwa Manispaa hiyo ambapo kwa mwaka kituo hicho kinakusanya shilingi Bilioni 5 kutoka kwenye vyanzo vyake ikiwemo ushuru wa kuingilia kituoni, vyooni, bajaji na pikipiki, hoteli inayosimamiwa na mzabuni, parking za kulaza magari, Ada ya kuingiza na kutoa mabasi kituoni na upangishaji wa fremu za biashara.
Sambamba na maelezo hayo wageni hao wamefanikiwa kujua namna kituo hicho kinaendeshwa na kusimamiwa kwa ufanisi kwa maslahi ya wanaubungo.
Nae Mhe. Kheri James Mkuu wa Wilaya ya Ubungo ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kwa uamuzi wake wa kutoka nje kuja kujifunza juu ya masuala mbalimbali yenye athari chanya kwa maendeleo ya wananchi wa Mtwara.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mhe. Selemani Nampanye ametoa shukrani kwa mapokezi mazuri waliyoyapata pamoja na fursa ya kujifunza mambo mengi mazuri yanayofanywa na Manispaa ya Ubungo na wameahidi kwenda kuyatekeleza kwa ukubwa katika Halmashauri yao.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa