Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Amos Makalla ameipongeza Manispaa ya Ubungo kwa usimamizi mzuri na wenye tija wa fedha za serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Makalla ametoa pongezi hizo leo julai 23, 2021 kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi kwenye jengo la utawala la Manispaa ya Ubungo na kueleza kuwa jengo hilo ni zuri sana na la kisasa hivyo watumishi wanawajibu wa kuhakikisha wanatoa huduma bora ili wananchi waridhike na kuipenda serikali yao.
Makalla amesema kuwa , amefungua mradi mkubwa kabisa wa jengo la utawala wa ofisi za manispaa hiyo ambao utatumia takribani bilioni 6.26 hadi kukamilika kwake ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni 1.99 ni za mapato ya ndani huku shilingi bilioni 4.3 zikitoka serikali kuu.
Mhe. Makalla ameipongeza Manispaa ya Ubungo kwa ukusanyaji mzuri wa mapato ya ndani hali inayowafanya waweze kutekeleza miradi mikubwa kwa kutumia mapato yake ya ndani.
Aidha, ameipongeza Manispaa ya Ubungo kwa maamuzi ya kutumia mfumo wa mafundi wenyeji yaani “Force Akaunti” baada ya kuvunja mkataba na mkandarasi alipewa kujenga jengo hilo kusuasua lengo ikiwa ni kuhakikisha miradi ya Serikali inakamilika kwa wakati na kwa viwango lakini pia kuhakikisha fedha ya serikali inatumika vizuri zaidi.
Mhe. Makalla ametumia wasaa huo kuipongeza Manispaa ya Ubungo katika kupambana na ugonjwa wa COVID 19 ambapo Watumishi wanachukua tahadhari kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka hali hii inazingatiwa kwa kiasi kikubwa, utoaji wa elimu kwa umma hasa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ikiwemo Kituo Kikuu cha Mabasi.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo, Mhe Jaffary Nyaigesha amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuweka jiwe la msingi katika mradi huo na kuahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi na ukusanyaji wa mapato bila kusababisha kero kwa walipa kodi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Beatrice R. Dominic ameishukuru Serikali ya awamu ya Tano na awamu ya Sita kwa kutoa eneo na fedha za kujenga jengo la ofisi na kusema kuwa jengo hilo lenye sakafu nne linauwezo wa kubeba watumishi 450 kwa wakati mmoja hali ambayo inarahisisha utendaji kazi katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa