Leo April 4, 2022 Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi katika Manispaa ya Ubungo lengo ikiwa ni kuangalia namna miradi hiyo inatekelezwa. Na kuelezea namna ambavyo amefurahishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika ziara hiyo Makalla ametembelea miradi iliyotokana na mgao wa fedha za Tozo za miamala Tsh Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Makuburi na Goba. Pamoja na miradi iliyotokana na mgao wa fedha za Mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari (SEQUIP) Tsh Milioni 940 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa sekondari mpya kwa Jimbo la Ubungo sekondari ya Ubungo plaza na Jimbo la Kibamba sekondari ya Msakuzi.
Akiongea katika ziara hiyo Makalla ameipongeza Ubungo kwa utekelezaji wa miradi hiyo na kwa jinsi wanavyoshirikiana vyema baina ya viongozi wa serikali na wa chama katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa ipaswavyo.
Aidha Makalla amesema ofisi yake itafanyia kazi maoni ya wananchi pamoja na viongozi ya kuomba mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari ya Ubungo iliyopangwa kujengwa katika eneo la kiwanja cha mpira kilichopo shule ya msingi Ubungo plaza isijengwe hapo kwani eneo hilo wamekuwa wakilitumia kwa michezo.
Makalla amesema amefurahishwa na ushirikiano alioupata wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo na amewataka watumishi wa serikali na viongozi wote wa Manispaa kuendelea kushirikiana na kuwasisitiza kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato.
Pia Makalla amesisitiza viongozi wote wa Manispaa hiyo juu ya ufuatiliaji wa shughuli za miradi, kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kuendelea kusimamia usafi wa mazingira, kuendelea kuyalinda maeneo ambayo machinga wameondolewa. Na ameitaka Manispaa hiyo kuweka mfumo wa POS mashine katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili kumuwezesha kuzifuatilia kwa umakini.
Nae Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Kheri James amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ujio wake na kuahidi kuwa maelekezo yote aliyoyatoa yatafanyiwa kazi na kutekelezwa ipaswavyo na kwamba Ubungo itaendelea kuwa ya mfano kwa nyanja zote.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa