Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh Amos Makalla amefanya kikao cha kuzindua zoezi la anuani za makazi na sensa kilichojumuisha madiwani, wenyeviti na watendaji wa kata na mitaa lengo ikiwa ni kuwa na uelewa wa pamoja wa juu ya umuhimu wa anuani za makazi ili kufanikisha zoezi la sensa.
RC Makalla ameeleza kuwa zoezi hilo litaanza tarehe 22/02/2022 na amewataka viongozi wa kata na mitaa kuongelea zoezi hili kila wanapofanya mikutano ya wananchi kwani zoezi hili litaenda kuwezesha zoezi la sensa ya watu na makazi ya 2022 kufanikiwa kwa ufanisi na ametaka zoezi hilo likamilike kabla ya tarehe 15 April 2022.
Mkuu wa Mkoa ameeleza miongoni mwa faida za zoezi hili ni kupunguza migogoro ya Ardhi, kuagiza biashara mtandaoni kwa urahisi, kurahisisha kuelekeza mgeni na kuweka mpangilio mzuri wa jiji, kuimarisha ulinzi na usalama na utambuzi wa maeneo ya huduma za kijamii.
Akizungumza wakati wa kikao hicho RC Makalla amewataka wenyeviti na watendaji kuhakikisha majina ya mitaa watakayoyachagua yanakuwa na heshima huku akitahadharisha zoezi lisiwe chanzo cha migogoro ya mipaka baina ya mtaa na mtaa.
Makalla amewataka viongozi hao kuhakikisha wanahitisha kikao na wamiliki wa hotel, na nyumba zote za wageni ili kuhakikisha siku ya sensa wageni wote waliolala kwenye nyumba hizo za wageni siku hiyo ya sensa wanahesabiwa.
Aidha RC Makalla amemshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuleta zoezi hilo litakaloifanya Tanzania kuwa na anuani ya kueleweka na hadhi ya kimataifa na amesema serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali il kuhakikisha vibao vya kuweka kwenye nyumba vinapatikana kwa gharama nafuu ambayo kila mwananchi ataweza kuimudu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Godwin Gondwe aliekuwa amemuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ilala kwa niaba ya wakuu wa Wilaya zote za Dar es Salaam amesema wapo tayari kupambana kwa hali na mali katika kuhakikisha zoezi hili linafanyika kama ilivyokusudiwa.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa