Timu ya uendeshaji wa huduma za afya Mkoa wa Dar es Salaam “RHMT” imefanya ziara ya usimamizi shirikishi Manispaa ya Ubungo na kutembelea kituo cha afya cha Sinza na Mbezi kwa ajili ya kuangalia utoaji wa huduma za afya katika vituo hivyo ikiwemo huduma ya lishe, dawa, huduma ya baba, mama na mtoto na uwepo wa vifaa na vifaa tiba.
Ziara hiyo imefanyika leo tarehe 21 Disemba, 2022 ambapo timu hiyo ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Rashid Mfaume imeipongeza Manispaa ya Ubungo kwa kuendelea kusimamia vizuri utoaji wa huduma za afya kwa usimamizi bora wa miradi, kuongeza vifaa tiba, uwepo wa dawa na vitendea kazi vyote kulingana na ngazi ya kituo cha kutolea huduma za afya.
Akiongea Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Mfaume amepongeza hatua za matayarisho ya kuanza kutoa huduma kwenye vituo viwili vipya ikiwemo kituo cha afya Goba na Zahanati ya Kinzudi ifikapo mwezi Januari, 2023 ambavyo vitasaidia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ubungo Dkt. Peter Nsanya ameahidi kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya ndani ya Manispaa hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vituo vipya vinaanza kutoa huduma ifikapo januari, 2023, kusimamia miradi, kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na utoaji wa elimu ya masuala mbalimbali ya afya.
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ina jumla ya vituo 22 vya kutolea huduma za afya ikiwemo Hospitali 1, vituo vya afya 5 na Zahanati 16 ambavyo vinaendelea kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa