Wananchi wa wilaya ya ubungo wamesisitizwa kujenga utamaduni wa kufanya usafi kwenye mazingira yao kila wakati na sio kwa sababu serikali imewataka kufanya hivyo ili kuepuka maradhi yanayotokana na kuwa na mazingira machafu ikiwemo magonjwa ya kuambukiza na mwonekano mbaya wa mji.
Wananchi wameelezwa hayo na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kheri James wakati waliposhiriki zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi ambapo kiwilaya zoezi hilo limefanyika katika Kata ya Kimara barabara ya Morogoro kuanzia Kimara Korogwe mpaka Kibo na kuwasisitiza kuwa Ubungo ina miundombinu mizuri hivyo ni wajibu wetu kuisafisha na kuipendezesha.
“Ubungo ni lango la jiji la Dar es Salaam hivyo tuitambulishe kwa kufanya usafi katika maeneo yote ikiwemo barabara kuu, mifereji, maeneo ya biashara na majumbani kwa kupanda miti, maua na kupaka rangi nyumba zetu” alisistiza Mhe. Kheri
Aidha, wamewakumbusha wamachinga wote kufanya biashara kwenye maeneo rasmi ili kupisha matumizi sahihi ya barabara lakini pia kupunguza madhara yanayotokana na kufanya biashara kwenye maeneo hatarishi.
Mhe. Kheri amewaeleza wananchi kuwa “Tambueni kuwa kufanya biashara kwenye maeneo yasiyo rasmi ni kosa kisheria hivyo anayekiuka hatua zitachukuliwa kama sheria inavyoelekeza ikiwemo kulipa faini”
Aidha, Mkuu wa Wilaya amewakumbusha wananchi kujitokeza na kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la Sensa ya watu na makazi itakayofanyika tarehe 23 Agosti, 2022 na kuwaeleza kuwa Sensa itasaidia Nchi kutoa huduma kulingana na idadi ya watu wa eneo husika.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa