Mapema Leo 15 Julai, 2022 Manispaa ya Ubungo imepokea Viti na meza za wanafunzi hamsini pamoja na miti kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Kimara kutoka STANBIC Benki ambayo inaendeleza Kampeni yao ya STANBIC Madawati Initiative.
Akiongea Nd. Omary Mtiga Mkuu wa kitengo cha wateja binafsi STANBIC, ameeleza kampeni yao imepanga kugawa madawati zaidi ya 1000 Tanzania nzima ili kuisaidia Serikali kupunguza changamoto ya madawati shuleni.
Ameendelea kueleza kuwa Sambamba na ugawaji wa madawati ambayo yanatokana na miti basi Benki hiyo imetoa mti mmoja kwa kila dawati moja ili kuendelea kutunza mazingira wakati huo huo kupunguza changamoto ya madawati.
Mtiga amesema STANBIC Benki imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa jamii kwani wanajamii ndio wateja wao wakubwa na kwamba wataendelea kushirikiana vyema na Serikali muda wowote pale ambapo watahitajika kufanya hivyo.
Nae Mhe. Kheri James Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, ametoa wito kwa Wadau wa mashirika mbalimbali kutoa misaada mbalimbali kwa jamii kama ambavyo STANBIC wamefanya kwani kufanikiwa kwao kunatokana na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa wanajamii.
Aidha, James ameendelea kueleza kuwa Serikali pekee haiwezi kutatua changamoto zote zilizopo kwa sekta mbalimbali hivyo Wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakiendesha vizuri biashara zao kutokana na mazingira mazuri waliyowekewa na Serikali yao basi wanapaswa kuisadia Serikali kwa nyanja mbalimbali.
James amewataka walimu na wanafunzi wa Shule hiyo kutunza madawati na miti ambayo imetolewa na Benki hiyo ikiwa ni ishara ya kutoa shukrani zao kwa Benki hiyo lakini pia kuvutia wadau wengine kutoa misaada mbalimbali katika Shule hiyo na Manispaa kwa ujumla.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa Shule hiyo Bi. Elizabeth Bonzo ameishukuru Benki hiyo kwa msaada huo na kuahidi kutunza misaada hiyo.
Bonzo ameeleza Shule hiyo inajumla ya wanafunzi 1585, na ina upungufu wa viti na meza za wanafunzi na walimu 621 hivyo upatikanaji wa viti na meza hizo imesaidia kupunguza changamoto hiyo.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa