Mapema Leo tarehe 06/07/2022 Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg. Beatrice Dominic amekutana na viongozi wa wamiliki wa mabasi (TABOA) wa Kituo cha Mabasi cha Magufuli (Magufuli Bus Terminal) lengo ikiwa ni kuweka mikakati ya pamoja na kudhibiti uwepo wa ofisi za kukatia tiketi nje ya kituo hicho.
Akiongea katika kikao hicho Ndugu Beatrice amewataka TABOA kushirikiana vyema na Manispaa ili kuhakikisha Mabasi yote yanayofanya kazi nje ya Kituo waache kufanya hivyo na badala yake wamiliki wote wa mabasi wanapaswa kuwa na ofisi ndani ya kituo hicho
Beatrice, ameendelea kuelezea kuwa uwepo wa ofisi za kukatisha tiketi nje ya kituo umekuwa ukipelekea Manispaa kupoteza mapato mengi takribani Mil 100 kwa mwezi, lakini pia uhalifu wa kusafirisha madawa ya kulevya umekuwa ukifanyika kwani gari hizo zimekuwa zikifanya safari bila kukaguliwa sababu haziingii ndani ya kituo.
Mbali na hilo Beatrice ameeleza uwepo wa ofisi hizo nje ya kituo cha mabasi umekuwa ukipelekea matatizo mengine mengi ya kihalifu ikiwemo raia kutelekezwa stendi wakiwa na tiketi feki walizopatiwa na ofisi zilizopo nje ya kituo.
Aidha, kikao hicho kimeazimia Viongozi wa TABOA wapeleke kwa Meneja wa Kituo hicho orodha ya majina na picha za wafanyakazi wao zikiwemo na za mawakala wao. Ili Manispaa iwatengenezee vitambulisha maalumu vitakavyo watambulisha ili kusaidia kutatua changamoto zilizopo.
Akiongea Meneja wa Kituo hicho Ndg. Isihaka Waziri amewataka viongozi hao kuacha tabia yakuwapa fedha watu wanawapelekea wateja ambao sio wafanyakazi wao kitu ambacho kinapelekea kusababisha uingiaji wa watu kiholela ambao wanaweza kuwa wahalifu kituoni humo.
Nae Mwenyekiti wa TABOA Ndg Abdallah Kiongozi ametoa pongezi zake kwa Manispaa na Meneja wa Kituo hicho kwa ushirikiano wanaoupata na kuahidi kuyafanyia kazi yote waliokubaliana kuyatekeleza na wapo tayari kutoa ushirikiano muda wowote pale inapobidi.
#UbungoYetuFahariYetu
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa