TAKUKURU imepewa mamlaka ya kuzuia na kupambana na rushwa kupitia sheria no 11 ya mwaka 2007 na katika kufanikisha hilo Leo tarehe 22/11/2022 ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Ubungo kwa kushirikiana na Manispaa ya Ubungo imetoa semina kwa Madiwani wa manispaa hiyo lengo ikiwa ni kuendelea kuwakumbusha juu ya uwajibikaji unaostahili.
Katika semina hiyo Waheshimiwa Madiwani wamefanikiwa kujifunza mada mbalimbali ikiwemo umuhimu wao juu ya Mapambano dhidi ya rushwa, maadili ya kiutendaji, majukumu na wajibu wao katika uendeshaji wa shughuli za Halmashauri.
Akiongea katika mafunzo hayo bi Dorothea Mrema Afisa TAKUKURU Mkoa wa kinondoni ameeleza kufanya kazi kwa mazoea, ukosefu wa huduma bora katika jamii, kutosimamia vyema miradi ya maendeleo kunapelekea kuwepo kwa mianya ya rushwa na amewataka viongozi hao kushirikiana vyema na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za rushwa, kufuata sheria, kanuni na taratibu ili kuzuia mianya ya rushwa.
Nae Ndg. George Mwendamseke Afisa mwandamizi maadili ya viongozi wa Umma amewataka viongozi hao kusimamia maadili katika uwajibikaji wao ikiwa ni pamoja na kuepuka migongano ya kimaslahi, na hivyo kuwepo kwa ufanyaji kazi na uwajibikaji wa pamoja kwa maslahi ya wananchi.
“Maslahi binafsi yakizidi kuliko maslahi ya Umma Nchi haitaweza kuendelea” alisisitiza Mwendamseke.
Kwa upande wake Ndg. Stephen Maximillian Sindagulu Mwakilishi kutoka ofisi ya Mkoa wa Dar es salaam ameeleza wajibu na majukumu ya Madiwani katika uendeshaji wa Halmashauri ikiwa ni pamoja na wajibu wa ukusanyaji wa mapato pamoja na kusimamia shughuli mbalimbali za halmashauri.
Aidha Mhe. Jaffery Nyaigesha Mstahiki Meya wa Manispaa ameipongeza ofisi ya TAKUKURU ya Wilaya hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yanawezesha Madiwani hao kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuahidi kutofanya kazi kinyume na utaratibu, sheria na kanuni zilizowekwa kwa maslahi ya wananchi wa Ubungo.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa