Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imeadhimisha siku ya Wazee duniani iliyosindikizwa na kaulimbiu isemayo “familia na jamii ishiriki kuwatunza wazee” kwa kutoa huduma mbalimbali kwa wazee ikiwemo upimaji wa afya na matibabu pamoja na kutoa kadi za bima ya afya (iCHF) ikiwa ni moja ya mkakati wa serikali wa kuboresha huduma za afya kwa wazee.
Utoaji wa huduma hizo za afya umefanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 1 hadi 2 oktoba, 2020 na kilele kufanyika tarehe 3 oktoba, 2020 katika viwanja vya mnazimmoja jijini Dar es salaam ambapo wazee walipata fursa ya kupimwa magonjwa kama macho, kisukari, shinikizo la damu , moyo pamoja na kinywa na meno pamoja na kupewa ushauri nasaa wa masuala mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya wazee wenzake kwenye maadhimisho hayo, Bibi Hafsa Ismail Yasile wa kata ya Makurumila Wilaya ya Ubungo, ameeleza kuwa siku ya wazee duniani imekuwa nzuri sana kwakwe kwani amepata fursa ya kupata vipimo vya maradhi mbalimbali ikiwemo sukari , moyo, shinikizo la damu na amegundulika kuwa na ugonjwa wa shinikizo la damu ambapo ameshauriwa kuanza matibabu mapema.
Bibi Hafsa amesema faida ya kushiriki maadhimisho hayo amepata huduma za afya bure jambo ambalo kwa wazee ni zuri ukizingatia wazee wengi hawana uwezo wa kifedha kugharamia matibabu yao wakati wote “kwa kufika kwenye maadhimisho ya siku ya wazee nimebahatika kupata bima ya afya ( iCHF) ambayo itanisaidia kupata matibabu bure mwaka mzima kwenye kituo chochote cha kutolea huduma za afya”
Aidha, Bibi hafsa amewasii wazee wenzake kujenga utamaduni wa kushiriki kwenye shughuli mbalimbali zinazowahusu wao ili waweze kujua mambo mbalimbali kwa ustawi wa maisha yao “ siku nyingine wanapopata wito wowote wawajibike kuitika badala kukaidi na kubaki kuilalamikia serikali kuwa haiwajali”
Kwa upande wake Mzee Abuu Juma Segamba kutoka kata ya Manzese Wilaya ya Ubungo ameipongeza Serikali kwa kuweka utaratibu wa upimaji na utoaji wa huduma za afya bure kwa wazee na ameomba utaratibu huu uwe endelevu.
Mzee Segamba amefafanua kuwa, miaka ya nyuma wazee walikuwa wakiachwa nyuma ila kuanzia mwaka 2018 mpaka mwaka huu wazee wamekumbukwa kwa kupewa kipaumbele kwenye mambo mbalimbali ikiwemo kwenye huduma za afya.
Mmoja wa wazee wakipata akifanyiwa uchunguzi kwenye maadhimisho ya siku wazee duniani iliyoadhimishwa kimkoa katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam leo tarehe 3 oktoba, 2020
Aidha Mzee Segamba ameeleza kuwa wazee hasa wanaume bado wameachwa nyuma kushirikishwa kwenye Nyanja ya utoaji maamuzi na utungaji wa sera ikiwemo kutokuwa na uwakilishi bungeni.
“Ukiangalia makundi kama ya wanawake, vijana na walemavu wamepewa kipaumbele katika bunge ambapo wanapata uwakilishi bungeni kupitia uwepo wa nafasi za viti maalumu lakini wazee hasa wanaume hatuna fursa hiyo, hivyo tunaiomba serikali itupatie fursa ya kupata uwakilishi vyombo vya maamuzi kuanzi kwenye mabaraza ya madiwani na bungeni kama yalivyo makundi ya wenzetu” ameomba Mzee Segamba.
Aidha mwakilishi wa wazee jijini Dar es salaam ametumia siku hii ya wazee kutoa rai kwa serikali kuweka sheria itakayowafanya watoto kuwajibika kuwatunza wazee na wasipotekeleza wachukuliwe hatua za kisheria kama makosa mengine, kwa kufanya hivyo familia itakuwa imeshiriki kwa vitendo kuwatunza wazee kama kaulimbui ya maadhimisho haya ya mwaka huu inavyosema “familia na jamii ishiriki kuwatunza wazee”
Tanzania inaungana na nchi nyingine za umoja wa mataifa kuadhimisha siku hii kwa mujibu wa Azimio la Umoja wa Mataifa Na. 49 ya Mwaka 1991 kila mwaka, lengo ikiwa kuhamasisha jamii kuweza kulinda na kutetea haki za wazee duniani kote pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili na kuweka mipango ya kuzitatua ili waishi kwa heshima, hadhi na kuthaminiwa.
IMEANDALIWA NA;
Kitengo cha habari na uhususiano
Halmashauri ya manispaa ya ubungo
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa