Leo tarehe 07/09/2022 Manispaa ya Ubungo imefanya kikao kazi kilichojumuisha Watendaji Kata na Mitaa, Maafisa Afya na timu ya wataalamu ya Manispaa hiyo lengo ikiwa ni kuweka mikakati ya ukusanyaji wa mapato ndani ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Akiongea katika kikao hicho Mhe Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo ameeleza kuwa watendaji wa Kata na Mitaa wana jukum kubwa la kuiwezesha Manispaa katika kufanikisha zoezi la ukusanyaji wa mapato kwani wanaostahili kuchangia mapato hayo ni wananchi ambao wapo katika mitaa yao.
Aidha Nyaigesha ameendelea kuwasisitiza Viongozi hao kuhakikisha kuwa wafanya biashara wote na wananchi kwa ujumla wanalipa kodi, tozo, ushuru na ada mbalimbali za Halmashauri ili kuweza kuisaidia Manispaa hiyo kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Dkt. Peter Nsanya ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Manispaa ya Ubungo imekasimiwa kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 32 kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali.
Nsanya amewataka watendaji hao kujua vyanzo wanavyopaswa kukusanya na kuvisimamia ipaswavyo ikiwa ni pamoja na kuweka “target” za mapato wanayopaswa kukusanya ndani ya mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Nae Afisa Biashara wa Manispaa hiyo Bi Mary Mwakyosi ameainisha vyanzo vya mapato vya Manispaa hiyo ikiwemo leseni za biashara na za vileo, ushuru wa huduma, vibali vya ujenzi na vya sherehe, Ada za taka ngumu na za ulinzi shirikishi, faini za kuvunja sheria na vinginevyo.
Kikao hicho kimeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuendelea kujenga uwezo kwa Watendaji wa Kata na Mitaa juu ya ukusanyaji wa mapato, kuwepo kwa Afisa biashara kwenye kila Kata, kutoa motisha kwa Mtendaji atakaefanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato.
Manispaa ya Ubungo hiyo katika mwaka wa fedha uliopita wa 2021/2022 Manispaa hiyo ilikasiniwa kukusanya shilingi Bilioni 23 lakini ilifanikiwa kukusanya shilingi Bilioni 27 Sawa na asilimia 118%.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa