Halmashauri ya Wilaya leo Jan 28, 2022, imetoa mkopo usio na riba wenye thamani ya Tsh bilioni 1.1 kwa vikundi 133 vya wajasiriamali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ikiwa ni utekelezaji wa sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kutenga asilimia 10 za mapato yake ya ndani.
Akiongea na wanavikundi hao kabla ya kuwakabidhi hundi Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mh Kheri James ameipongeza Manispaa ya Ubungo kwa kutekeleza sera hiyo kwa vitendo ambapo wanufaika 1201 wamewezeshwa mikopo isiyo na riba ambayo itawasaidia kuongeza mitaji kwenye biashara zao na hivyo kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla
“Mikopo hiyo itumieni vizuri kukuza biashara zenu kwa sababu haina riba tofauti na ukikopa benki ambapo kuna riba kubwa, utoaji wa fedha hizi ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata fursa ya kumiliki biashara”.
Aidha James ameendelea kuvisisitiza vikundi hivyo kutumia pesa hizo kukuza biashara zao na sio matumizi mengine na matumizi hayo yaende sambamba na urejeshwaji wa pesa hizo ili kuwapa wengine fursa ya kukopeshwa.
Kheri amevisisitiza vikundi vya vijana kurejesha pesa hizo kwa wakati kwani wenyewe wamekuwa na changamoto katika urejeshaji wa fedha hizo tofauti na vikundi vya akina mama.
Pia amewaomba maafisa maendeleo ya jamii kuwa na utaratibu wa kuvitembelea vikundi hivyo mara kwa mara na sio tu kuishia kuvipa mikopo ili kuvishauri na kuongeza ufanisi katika shughuli zao na amevisisitiza vikundi hivyo umuhimu wa kuzingatia taratibu za fedha, na kulinda umoja na mshikamano katika vikundi vyao na Taifa kwa ujumla.
Katika mikopo hiyo ya Tsh bilioni 1.1 jumla ya vikundi 133 vyenye wajasiriamali wapatao 1201 wanaenda kupatiwa mikopo ambapo vikundi vya wanawake 85 watapatiwa Tsh Milioni 643, vikundi vya vijana 42 watapatiwa Tsh Milioni 429 na jumla ya Tsh Milioni 74 zitatolewa kwa vikundi vya watu wenye ulemavu.
“UBUNGO YETU FAHARI YETU”
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa