Kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Polio uliotokea nchi jirani, Manispaa ya Ubungo Leo tarehe 01 Disemba, 2022 imefanya uzinduzi wa nyumba kwa nyumba wa chanjo ya matone ya polio kwa watoto wenye umri kuanzia mwezi sifuri hadi miaka mitano.
Akiongea katika uzinduzi huo Dkt. Peter Nsanya ameeleza kampeni hiyo ya kitaifa ya awamu ya nne itafanyika kwa siku nne ambapo wataalamu wa afya watapita nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kuwapatia chanjo ya matone ya polio kwa watoto wenye umri wa kuanzia miezi 0 hadi miaka 5. Pia amesema watoto waliokwisha pata chanjo hiyo kwa awamu za nyuma bado watatakiwa kupata kwa awamu hii kwani chanjo hiyo haina madhara.
Dkt. Peter ameeleza ugonjwa wa polio unatokana na kula chakula chenye kinyesi na madhara yake ni kupata ulemavu wa kudumu au kupoteza maisha hivyo ametoa wito kwa jamii kuhakikisha kuwa mazingira yanakuwa safi na chakula kinaandaliwa kwa usafi muda wote.
Nae Mhe. Kheri James Mkuu wa Wilaya ya Ubungo amesema kila mzazi au mlezi mwenye mtoto mwenye kustahili kupata chanjo ana jukumu la kuhakikisha mtoto anapata chanjo hiyo kwa kuwapa ushirikiano watoa huduma watakao pita majumbani kwao.
Aidha, James ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa inawalinda watu wake ili wawe salama kwa mashambulizi ya magonjwa yaliyopo ndani na yale yanayotoka nje na ameeleza hakutakuwa na mtoto mwenye kustahili kupata chanjo na akaachwa bila kupata chanjo.
“Ni jukumu la Serikali na ni wajibu wa Serikali kuendelea kuwatunza, kuwalinda na kuhakikisha watoto wetu wanakuwa katika mazingira yenye afya na hatimae kuwa bora katika kizazi cha Leo na cha kesho kwa maslahi ya Nchi yetu” Alisema James.
Manispaa ya Ubungo kwa awamu ya nne ya kampeni ya chanjo ya matone ya polio inategemea kuwapatia chanjo hiyo ni takribani watoto 209,688.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa