Viongozi wa Wilaya ya Ubungo wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Madiwani na Wataalam wa Manispaa ya Ubungo wamejengewa uwezo kuhusu mfumo wa anwani za makazi lengo ikiwa ni kuwa na uelewa wa pamoja katika kulitekeleza zoezi hilo muhimu.
Akiongea wakati wa kufungua mafunzo hayo yaliyotolewa leo Februari 22, 2022 kwa viongozi hao, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mheshimiwa Kheri James ameeleza kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa utoaji wa elimu kuhusu zoezi hilo kwa viongozi wa ngazi mbalimbali ambao ndio wasimamizi wakuu wa zoezi.
Tumeitana hapa ikiwa ni utekelezaji wa azima ya Serikali ya kujengeana uwezo kama viongozi tunaowajibika kusimamia zoezi la mfumo wa anwani za makazi ili kila mtu ajue wajibu wake katika zoezi hili ambalo litatekelezwa kwa muda mfupi yaani kama “operational” tunatamani zoezi hili lifanyike kwa ufanisi na kwa haraka ikiwezekana tuwe wa kwanza kumaliza.
Aidha, Mhe James amewaeleza Madiwani kwa nafasi zao wanawajibu mkubwa sana katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi hilo kwa kutoa ushirikiano wa kutoa taarifa zinazohitajika wakati wa wakusanya taarifa hizo wakifika kwenye nyumba zao kwa ajili ya kuwekwa kwenye mfumo.
“Tambueni kuwa kufanikisha zoezi hili la mfumo wa anwani ni kufanikisha zoezi la Sensa linalotarajia kufanyika mwaka huu ambapo mazoezi hayo yote yanatekelezwa kwa mujibu wa sheria” alisisitiza Mhe. James”
Akiongea wakati wa kutoa mafunzo hayo, Mratibu wa zoezi hilo JOHN ILOMO alieleza kuwa katika uundaji wa anwani za makazi unahusisha nambari za nyumba, postkodi na majina ya barabara na kusistiza kuwa utoaji wa majina hayo uzingatie historia ya eneo pamoja na matamshi yanayokubalika na mtaa husika, huku majina yenye itikadi za kidini, kikabila na kisiasa yakikatazwa kabisa kutumika.
Ilomo amesema kuwa utoaji wa anwani za makazi kwa maeneo yasiyopangika namba zitatolewa bila kufuata mtiririko tofauti na zile zilizopangika ambapo utoaji wa anwani wake utazingatia utaratibu wa namba shufwa kwa upande kulia na namba witiri kwa upande wa kushoto wa barabara.
Pia ameendelea kuwaeleza viongozi hao kuwa maeneo hatarishi au yasiyorasmi kama hifadhi ya barabara, mkondo wa maji au chini ya nguzo ya umeme sheria imekataza kutoa anwani za makazi hivyo taarifa zao hazitaingizwa kwenye mfumo huu.
Kwa upande wao Madiwani wameipongeza serikali kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamewapa fursa ya kujua nini cha kuwaeleza wananchi namna ya kushiriki kwenye zoezi hilo muhimu la kitaifa ili likamilke kwa wakati na hatimaye malengo ya serilaki yatimie ikiwemo la kuongeza wigo wa ajira kwa njia ya mtandao, kuwezesha ukusanyaji wa mapato, kusaidia zoezi la sensa kwa wepesi na kupanga vizuri mipango ya maendeleo halisi inayotekelezeka Nchi nzima.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa