Wakandarasi wa vibao vya Anwani za Makazi wapewa siku saba kukamilisha zoezi lote la uwekaji wa nguzo na vibao vya anwani katika mitaa yote iliyosalia kwa Manispaa ya Ubungo. Hayo yameelezwa na mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe Kheri James Leo Juni 28, 2022 alipofanya kikao na wenyeviti wa mitaa, watendaji wa kata pamoja na wakandarasi wa vibao vya Anwani za makazi kwa Manispaa ya Ubungo kujadili utekelezaji wa zoezi pamoja kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Katika kikao hicho Mhe. Kheri amewasisitiza wenyeviti wa mitaa pamoja na watendaji wa mitaa na kata kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ukusanyaji wa fedha za vibao ambazo zilipitishwa na kukubalika kwenye vikao halali vya mitaa vilivyofanyika mapema mwanzoni mwa zoezi hilo.
Aidha, Mhe. Kheri ametoa maelekezo kwa wakandarasi wa vibao kuhakikisha wanaendelea na zoezi la kubandika vibao hivyo katika mitaa yote ambayo haijakamilika huku ofisi ya Mkuu wa Wilaya ikiandaa mikataba ya malipo baina ya Wenyeviti wa mitaa na wakandarasi ili kushughulikia malipo yote kwa wakati. Mpaka sasa kata ambazo bado ziko nyuma kwenye ukamilisha wa zoezi hilo ni pamoja na Mburahati, Saranga, Goba, Msigani na Kwembe
“Hakikisheni mnafanya kazi ya Wenyeviti wangu kwa kubandika vibao kila nyumba na kila mtaa pamoja na nguzo kwenye kila barabara, na mimi nitashirikiana na wenyeviti wangu kuhakikisha malipo yenu yanakamilika kwa wakati” alisema
Sambamba na hilo, Mhe. Kheri amewaagiza watendaji wa mitaa na kata kutokukaa ofisini kwa siku saba kuanzia leo na badala yake wawepo mitaani kwenye kukamilisha zoezi hilo. Hayo ameyasema baada ya kubainika changamoto kubwa kwenye zoezi hili ni kuwa baadhi ya wakandarasi wanalega lega kutokana na uwezo mdogo wa uzalishaji wa vibao, hivyo Mhe. Kheri amewataka wenyeviti, watendaji wa kata na mitaa kuwepo mitaani kutoa elimu ya zoezi hilo pamoja na kukusanya fedha za vibao
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Ndugu Beatrice Dominic amemshukru Mkuu wa Wilaya kwa kuendelea kusimamia zoezi hilo kwa ukaribu na amemuahidi kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na kuwa ndani ya siku saba kutoka leo zoezi hilo litakua limekamilika.
#UbungoYetuFahariYetu
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa