Mkurugenzi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI , Julius Nestory amewaagiza watendaji wa sekta ya elimu Manispaa ya Ubungo jijini Dar Es salaam kuhakikisha wanawasimia walimu wa shule za msingi na sekondari kufundisha wanafunzi kwa ufanisi ili kuzalisha wasomi wenye ueledi wa kutosha kwa ajili ya maendeleo ya Taifa na wanaoweza kushindana na mataifa mengine kitaaluma.
Agizo hilo amelitoa leo tarehe 16 februari, 2021 kwenye kikao kilichojumuisha viongozi watendaji wa elimu za msingi na sekondari , waratibu elimu kata, walimu wakuu, na wakuu wa shule wa Manispaa hiyo lengo likiwa kukumbushana wajibu wao katika kutoa elimu bora kwa watoto ambao ni Taifa la kesho.
Wataalamu wa elimu manispaa Ubungo wakiwa kwenye kikao cha kupokea maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi wa elimu OR_TAMISEMI
Nestory ameeleza kuwa malengo mahususi ya kikao hicho ni kuwakumbusha walimu kuwa elimu wanayotoa darasani ilenge kuwaongezea maarifa yatakayodumu kwa muda mrefu lakini pia yawasaidie kutatua changamoto zake za kimaisha.
Akiainisha hatua tano mhimu za kuzingatia katika ufundishaji bora, Nestory amesema kuwa mwalimu lazima awe na muhtasari wa somo,nukuu ya somo, andalio la somo pamoja na kufanya tathimini ya mada husika ili kujua uelewa wa wanafunzi kwenye somo husika.
"Waratibu elimu kata, Wakuu wa shule na Walimu wakuu simamie maandalio ya masomo kwa walimu wenu kwani hatua moja ikirukwa ufundishaji wa ufanisi hautakuwepo na hivyo kuzalisha wanafunzi wenye uelewa mdogo na wasioweza kushindana katika soko la kimataifa" alisisitiza Nestory
Tatizo kubwa lipo kwenye ukaziaji hafifu wa maarifa ,walimu fundisheni kwa makini na mawanda mapana na kuchagua vitu mhimu na kuwajengea uelewa zaidi ili viwasaidia kujibu vyema mitihani yao na hatimaye kuongeza ufaulu.
Nestory ameeleza kuwa kwa elimu ya msingi walimu wahakikishe wanatumia mbinu bora ikiwemo kuwa na madarasa yanayoongea zitakazomwezesha watoto kujua kusoma, kuandika na kuhesabu vizuri kabla ya kufika darasa la nne.
Aidha kwa upande wa sekondari, Nestory amesisitiza walimu kutumia lugha ya kiingereza wakati wa kufundisha ili kuwasaidia watoto kujifunza lugha hiyo ambayo ndio wanayotumia kufanya mitihani yao " wanafunzi wengi wanafeli mitihani kwa kushindwa kujieleza kwa ufasaha wajengeeni uwezo kwa kuweka mikakati ya kuhakikisha wanaongea lugha hilo muda wote wakiwa shule"
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar Es salaam ndugu Abdul Maulid amewasisitiza walimu wa sekondari kufuata miongozo ya ufundishaji ikiwemo kutumia lugha ya kiingereza kufundishia pamoja na kutumia wiki nane za mwanzo kunajengwa uwezo wanafunzi wa kidato cha kwanza ili kuwajenga kisaikologia juu ya matumizi ya lugha hiyo ambayo ni tofauti na shule ya msingi walikotoka.
Wakitoa kauli kwa nyakati tofauti walimu Wakuu na wakuu wa shule wameahidi kutekeleza maagizo hayo kikamilifu ambayo yanalenga kuboresha elimu kwa wanafunzi na kuongeza ufaulu.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa