Manispaa ya Ubungo kwa kushirikiana na shirika la SOS CHILDREN VILLAGE Leo September 10, 2022 wametoa mafunzo kwa wataalamu wa Manispaa hiyo wakiwemo Maafisa Watendaji Kata, Ustawi wa jamii, Maendeleo ya Jamii, pamoja na Maafisa Ustawi wa Jamii wa vituo vya Polisi lengo ikiwa ni kuwapa mafunzo juu ya masuala ya Malezi Mbadala ya watoto.
Kumekuwa na sababu mbalimbali zinazopelekea mtoto kupelekwa kwenye malezi mbadala ikiwemo ukatili na unyanyasaji wa watoto, wazazi kufariki na kupelekea mtoto kukosa uangalizi, imani potofu na mengineyo.
Sheria ya mtoto No 21 ya mwaka 2009 ambayo imefanyiwa maboresho mwaka 2019 imetoa wajibu kwa Serikali, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuwalinda watoto dhidi ya ukatili na ubaguzi.
Akiongea katika mafunzo hayo Bi Edna Kamaleki anaeshughulika na masuala ya ushauri wa haki za watoto (Adv & Child Right Consultant) ameeleza kuwa malezi mbadala ni malezi ambayo mtoto anayapata akiwa chini ya uangalizi tofauti na familia yake au malezi yake ya asili, ambayo mtoto anayapata kutoka kwenye aina mbalimbali ikiwemo malezi ya makao, kuasili, kambo, ndugu na ya watu wa kuaminika.
Nae Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dkt. Peter Nsanya wakati anafungua mafunzo hayo amewataka wataalamu hao kuzingatia mafunzo hayo na ametoa wito kwa jamii juu ya watu wote wanaowapatia watoto malezi mbadala wakiwemo watu wa kuaminika, ndugu, wanaoasili watoto, makao yanayolea watoto na malezi ya kambo kulea watoto hao kwa kuzingatia misingi, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuwa na Jamii salama.
Kwa upande wake Bw. Godson Tony mwakilishi kutoka shirika la SOS CHILDREN’S VILLAGE ameeleza kuwa shirika hilo kwa kushirikiana na Serikali limeandaa mradi wa kumuwezesha mtoto kuanzia hatua ya kumhudumia hadi kumuunganisha na familia yake pale itakapohitajika kufanya hivyo.
Mkuu wa kitengo cha Ustawi wa Jamii wa Manispaa hiyo Bi. Zainabu Masilamba amewataka Maafisa Ustawi Kata wa Manispaa hiyo kuzitambua makao ambazo zina watoto wanaostahili kukabidhiwa kwenye familia zao za asili na kuwapa maelekezo wahusika wa Makao hizo juu ya taratibu za kufuata juu ya watoto hao.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa