Leo Machi 30,2022 Wizara ya Afya na Ofisi ya Raisi - TAMISEMI wamefanya kikao kazi na timu ya kusimamia Mpango wa ugawaji wa vyandarua mashuleni (Schools Net Program - SNP) ya Manispaa ya Ubungo kwa Shule za Msingi za Serikali na Binafsi za Manispaa ya hiyo lengo ikiwa ni kuendeleza mkakati wa kudhibiti kuenea Malaria Nchini.
Akiongea katika kikao hicho Mtaalamu kutoka Wizara ya Afya Ndugu Peter Gitanya ameeleza kuwa Serikali imeweka mipango ya kudhibiti kuenea kwa Malaria kwa kuhakikisha wananchi wanapata vyandarua kwa 80% hadi kufikia 2030 na kupunguza malaria kwa 3.5% hadi kufikia 2025.
Gitanya ameeleza kuwa zoezi hilo kwa sasa linatekelezwa kwa kugawa vyandarua katika Shule zote za Msingi za Serikali na Binafsi kwa wanafunzi wote waliosajiliwa na wasiosajiliwa na kwamba wakuu wa shule wanapaswa kumaliza kugawa vyandarua hivyo ndani ya siku 3 mara baada ya kuvipokea kutoka Bohari ya Dawa (MSD).
Aidha, Gitanya amewataka Wataalamu wa timu hiyo kuhakikisha Walimu Wakuu wanatuma taarifa sahihi za idadi ya wanafunzi wote waliopo katika shule zao pamoja na kuandaa taarifa sahihi wakati wa kupokea na kugawa vyandarua hivyo.
Kwa upande wake Mtaalamu kutoka Ofisi ya Raisi - TAMISEMI Stella Kajange amewasisitiza Wataalamu ngazi ya Manispaa kusimamia vizuri zoezi kwa kutumia fedha vizuri, kufanya ufuatiliaji wa karibu, kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kutumia vyandarua na kufanya tathmini ni kwa kiasi gani vyandarua hivyo vimeenda kufanya kazi iliyokusudiwa ili kufikia lengo la Serikali la kudhibiti kuenea kwa Malaria.
Akiongea kwa niaba ya Timu ya Manispaa Lucy Shirima ameipongeza Serikali kwa mpango huo wa kudhibiti Malaria Nchini na kuahidi kuwa timu hiyo itatekeleza zoezi hilo ipasavyo ili kufanikisha zoezi hilo la kitaifa.
Manispaa ya Ubungo inajumla ya Shule za Msingi 187 ambapo Shule za Msingi za Serikali 66 na Shule za Msingi Binafsi 121 zenye Jumla ya Wanafunzi 142,458.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa