Timu ya wataalamu ya Manispaa (CMT) chini ya Mkurugenzi wa Manispaa ndugu Beatrice Dominic wametakiwa kujipanga vizuri kwenye usimamiaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa ndani ya Manispaa ya Ubungo. Hayo yamesemwa leo Machi 01, 2023 na mkuu wa wilaya ya Ubungo Mhe.Hashim Komba wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi
Ziara hiyo imefanyika leo ambao Mhe. Komba aliambatana na kamati ya ulinzi na usalama pamoja na timu ya wataalamu wa Manispaa ya Ubungo ambapo miradi iliyotembelewa ni pamoja na shule ya msingi Kiluvya, shule ya msingi Kibamba, kituo cha Afya Amani, shule maalumu ya wasichana, kituo cha Afya Goba, ujenzi wa shule ya sekondari Ubungo NHc pamoja na kituo cha Afya Palestina
Katika ziara hiyo Mhe. Komba ameridhishwa na maendeleo ya baadhi ya miradi ikiwemo shule ya msingi Kiluvya ambapo pamejengwa madarasa matatu kwa shilingi 60,000,000 fedha za mapato ya ndani pamoja na mradi wa ujenzi wa shule maalumu ya wasichana ya mkoa ambayo inajengwa kwa gharama za shilingi bilioni 3 fedha kutoka serikali kuu
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Hashimu Komba akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi katika shule ya msingi kibamba
Aidha katika mradi wa madarasa matatu katika shule ya msingi Kibamba ambayo yalikabidhiwa mwezi Disemba 2022 kwa ufadhili wa kanisa la Yesu Kristo watakatifu wa siku za mwisho, Mhe. Komba hajaridhishwa na ubora wa madarasa hayo na tayari ametoa maagizo kwa mkurugenzi kuchukua hatua za kurekebisha dosari zilizojitokeza
Katika mradi wa shule ya sekondari Ubungo NHC ambao panajengwa madarasa 8 kwa mtindo wa ghorofa, Mkuu wa Wilaya pamoja na kamati yake ya Ulinzi na Usalama imebaini dosari katika mfumo wa manunuzi na matumizi na tayari ameagiza TAKUKURU na Mkaguzi wa ndani kuanza uchunguzi mara moja
Kwa upande wa shule maalumu ya wasichana ambayo inajengwa mtaa wa Njetemi Kwembe, Mhe Komba ameridhishwa na maendeleo ya mradi huo ambao unatarajiwa kukabidhiwa mwezi Aprili 2023.
Pamoja na hilo Mhe. Komba ameiagiza idara ya Mazingira kufika katika mradi huo na kuandika andiko la kupendezesha eneo lote la shule pamoja na idara ya mipango miji kuandaa michoro ya miundombinu wezeshi ya kuunganisha jengo moja na jengo jingine
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa