Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kheri Denice James amewataka wawezeshaji wa mpango wa TASAF kipindi cha pili awamu ya tatu kuzingatia kanuni taratibu na miongozo iliyowekwa katika zoezi la uibuaji wa kaya masikini katika Wilaya hiyo ili kuwafikia walengwa wanaostahili.
Kheri amewaeleza wawezeshaji hao wa ngazi ya mtaa leo Julai 6, 2021 kwenye kikao kazi cha kujenga uelewa kuhusu mpango huo wa kunusuru kaya masikini kipindi cha pili kwa viongozi, Watendaji na wawezeshaji na kueleza kuwa kazi hiyo ni mhimu sana katika kupunguza umasikini kwa wananchi watakaokuwa na sifa za kuingia kwenye mpango.
Kheri amesema "Nasisitiza kila aliyepewa kazi hii atafanya kwa uaminifu na uadilifu mkubwa ili kufikia lengo la Serikali la kupunguza umasikini kwa wananchi wetu kupitia mpango huu, kawahudumieni kwa upendo na haki"
Akitoa maelezo mafupi kuhusu mpango huo mbele ya washiriki wa mafunzo hayo mwakilishi wa Mkurugenzi mtendaji wa TASAF Tunu Munthali amesema, kwa kipindi cha awamu ya tatu ya mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAFIII) kinatekelezwa katika Halmashauri zote184 na za Tanzania Bara na Wilaya zote za Zanzibar.
Munthali ameeleza kuwa, katika kipindi hiki cha mpango kitaifa, TASAF inatarajia kufikia Kaya milioni moja laki nne na hamsini elfu (1,450,000) zenye wanufaika zaidi milioni saba (7,000,000) nchi mzima.
Aidha, katika kipindi hiki mpango utakikita zaidi kuongeza na kuboresha huduma za jamii ikiwemo kuendeleza rasilimali watoto hususani katika upatikanaji wa Elimu na Afya huduma ambazo ni mhimu katika ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla
Wanufaika wa mpango huu ni Kaya zote zinazoishi maisha duni ikijumuisha watoto chini ya miaka mitano wanaohudhuria kliniki,wanafunzi wa shule za awali, Msingi na Sekondari, wajawazito na wanakaya wenye ulemavu ambapo ruzuku watakazopokea ni ya Msingi na ya kutimiza masharti ya Elimu na Afya.
Aidha, katika mpango huo, kutakuwa na ajira zitazotokana na utekelezaji wa miradi itakayoiburiwa na walengwa kwenye maeneo yao ambazo zitawapa ujira.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Beatrice Dominic ameishukuru TASAF kwa mpango huu ambao utafanyika kwenye Mitaa yote ya Manispaa hiyo na kuahidi kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mpango huo ili ulete tija katika kupunguza umasikini kwa wananchi.
Luguruni Area, Morogoro Road
Sanduku la Posta: P. 0. BOX 55068 Dar es Salaam
Telephone: +255 22 2926341
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: md@ubungomc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.Haki zote zimehifadhiwa